Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara wilayani Busega siku ya tarehe 6 Machi 2020. Katika ziara hiyo ya siku moja wilayani Busega, makamu wa rais aliambatana na Naibu Waziri waFedha, Mhe. Dr.Ashatu Kijaji, Naibu Gavana Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dr.Bernad Kibese, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe na kupokelewa na wenyeji wao mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka, mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Busega.
Katika ziara hiyo makamu wa rais alipata fursa ya kufungua tawi la Benki ya NMB-Busega na kuwataka wananchi kutumia huduma za kibenki ikiwemo kuhifadhi fedha na kuomba mikopo kwaajili ya kuinua uchumi ili kuleta maendeleo wilayani Busega.
Mhe. Makamu wa rais amesisitiza kuwa na tija ya kuleta maendeleo kwa benki kuweza kusaidia jamii katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo elimu, kilimo na ufugaji katika wilayaya Busega. Ameiomba Benki ya NMB kuendelea kuwa mdau mkubwa wa maendeleo na kuwataka waendelee kuwekeza ili kuzidi kusaidia wananchi kwenye nyanja nyingi ikiwemo elimu na afya.
Awali, mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Antony Mtaka aliishukuru Benki ya NMB kwa mchango wanaotoa katika mkoa wa Simiyu ikiwemo magodoro kwa shule za sekondari na vifaa vya ujenzi wa madarasa na kuomba ushirikiano huo uzidi kuendelea.
Aidha, mkuu wa wilaya ya Busega, alimshukuru makamu wa rais kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kusimamia maendeleo mbalimbali na kumuomba azidi kusimamia shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo wilaya ya Busega ili wilaya iwe na maendeleo yanayoendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano.
Mheshimiwa makamu wa rais, anafanya ziara ya siku tatu mkoa wa Simiyu kuanzia tarehe 6-8 Machi 2020, na pia anatarajia kuwa mgeni rasmi katika kilele cha siku ya wanawake duniani ambayo kitaifa inafanyika mkoa wa Simiyu.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa