Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Busega limeidhinisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya Shilingi bilioni 31.096. Kikao cha baraza hilo kimefanyika tarehe 13 februari, 2023 katika ukumbi mdogo wa Halmashauri.
Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 9.09 ni kwaajili ya Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo, Shilingi bilioni 18.74 ni Mishahara, Shilingi milioni 951.07 Ruzuku ya Matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 2.30 ni mapato ya ndani.
Akiwasilisha taarifa ya bajeti hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuari ya Wilaya ya Busega Bw. Ogada Magati, ambae ni Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu amevitaja vipaumbele 8 ambavyo ni katika Sekta za Afya, Elimu Msingi na Sekondari, Utawala, Mifugo na Uvuvi, Ardhi, Maliasili na Uhifadhi Mazingira, Kilimo na Mipango na Uratibu.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe ametoa rai kwa wataalam kuhakikisha wanatimiza kile kilichopo kwenye bajeti hii. “Bajeti hii imefuata zaidi uhalisia, naomba tuitekeleze kwa uadilifu mkubwa na kujitoa kwaajili ya wananchi wa Busega”, aliongeza Sundi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Anna Gidarya amesema ili kutimiza vyema bajeti hii ni lazima tuhakikishe tunasimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani. Aidha Gidarya amewataka madiwani kuendelea kusimamia ujenzi wa miradi mbalimbali katika maeneo yao.
Bajeti hii ya mwaka wa fedha 2023/2024 imepanda kutoka Shilingi bilioni 31.057 ya mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia Shilingi bilioni 31.096.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa