Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesuluhisha mgogoro wa shamba la kijiji uliodumu zaidi ya miaka 15 katika kijiji cha Nyamikoma A, ambapo baadhi ya wananchi walivamia sehemu ya shamba hilo na kujimilikisha. Takribani ya ekari 6.1 zimeweza kurejeshwa kama mali ya kijiji hicho.
Akiongea katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho siku ya tarehe 10 Januari, 2023, Zakaria amesema suluhu iliyofikiwa haikuwa ya kutafuta nani chanzo bali ni maelewano na taratibu zote zimefuatwa. “Wengi waliamini kwamba hili halitawezekana bila kukamata watu, ambao pengine walionekana ni kikwazo katika hili, tumejaribu kufanya jambo hili kwa umakini wake na taratibu zimefuatwa ili badae asitokee mtu akasema ameonewa, na leo tumefikia suluhu ya mgogoro huu”, aliongeza Zakaria.
Wananchi wa kijiji hicho wameupongeza uongozi wa Wilaya ya Busega kwa kutatua utata uliodumu kwa muda mrefu, ambao umekuwa ukishindikana mara kwa mara, hivyo wameiomba Serikali kuendelea kusimamia haki za wanyonge ambao hawafahamu sheria na taratibu mbalimbali. “Kiukweli tumefarijika sana kwa hili na hii ndio haki kwani shamba la kijiji ni mali ya wananchi wote na sio mali ya mtu mmoja”, alisema mwananchi mmoja aliyeshiriki mkutano huo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Kulwa Bula amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kazi kubwa aliyoifanya na kusimamia suala hilo ambalo lilikuwa ni kero kwa uongozi wa Serikali ya kijiji. “Wengi waliamini tunatetea watu waliovamia shamba la kijiji lakini sio kweli na leo haki imetendeka, uongozi wa Serikali ya kijiji utaendelea kusimamia shamba hilo na hakuna atakayevunja sheria ya kuvamia tena shamba hilo”, alisema Bula.
Aidha, Zakaria ameagiza kupimwa kwa shamba hilo ili kupata uhalisia wa ukubwa wa shamba hilo ikiwa ni sehemu ya mali halali ya kijiji hicho. Pamoja na mambo mengine, Zakaria amewataka wazazi wahakikishe wanawapeleka watoto shule kwani hilo ni jukumu la kila mzazi, huku akiwaasa matapeli ambao wameanza kujitokeza katika baadhi ya maeneo kuacha tabia hiyo mara moja kwani atakayebainika hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi yao.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa