Uzinduzi wa upuliziaji wa viwatilifu kwenye madimbwi ya maji ili kuangamiza mazalia ya Mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria umefanyika katika kituo cha afya NASSA na kuhudhuriwa na Mwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya, David Pallangyo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Godfrey Mbangali, watumishi wa Afya na Maafisa afya kutoka kata zote 15. Zoezi hilo litakalochukua siku nne kuanzia tarehe 17 hadi 20 Juni, 2020 litafanyika katika kata zote 15 na vijiji vyote 59 vilivyopo wilayani Busega.
Mwakilishi kutoka ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Busega, David Pallangyo, amewataka wananchi kutoa ushirikiano na kuacha fikra potofu juu ya zoezi hilo. Amesisitiza kuwa dawa zinazotumika katika zoezi hilo la kuua mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria hazina madhara yoyote kwa afya ya binadamu hivyo wananchi watoe ushirikiano ili kukamilisha kusudio la zoezi hilo.
Awali Mganga Mkuu wa Wilaya ya Busega Dkt. Godfrey Mbangali, akimkaribisha mgeni rasmi amesisitiza kuwa zoezi hilo la kupulizia dawa kwenye mazalia ya mbu lililofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la T-Marc Tanzania wanaoshughulika na mradi wa badili tabia tokomeza Malaria kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto litafanyika kwenye kata zote 15 kwa siku nne, na litahusisha sehemu zenye maji yaliyotuama ambazo ndizo sehemu kuu za mazalia ya mbu wa malaria.
Ugonjwa wa Malaria ni moja ya magonjwa yaliyo na maambukizi makubwa wilayani Busega. Kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2018 hali ya maambukizi ya Malaria kwa jamii ya Busega ilikuwa ni 8.3% ambapo ilikuwa ya pili kimkoa kuwa na maambukizi ya juu, huku katika kipindi cha miaka mitatu maambukizi ya Malaria kwa wilaya ikiwa 45,719. Hivyo kuzinduliwa kwa zoezi hilo kutasaidia kupunguza maambukizi ya malaria wilayani Busega.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa