Suala la malipo ya posho kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji ni moja ya jambo lililochukua nafasi wakati wa kikao cha baraza la madiwani robo ya tatu, Januari-Machi kilichofanyika 03/06/2020, huku madiwani wakitaka kujua hatma ya malipo hayo kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji.
Diwani wa kata ya Igalukilo, Mhe. Charles Lukale aliomba kujua mwenendo wa malipo ya posho kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji pia ni lini madeni ya baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji yatalipwa. Akitoa ufafanuzi wa jambo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Anderson Njiginya Kabuko, amesema posho na baadhi ya madeni ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji yanatambulika na tayari malipo ya madeni yanaendelea kufanyika kwa baadhi ya kata hivyo hakuna shaka kuhusu suala hilo la malipo.
Kabuko aliongeza; “tumeazimia kulipa posho ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kutokana na mapato yanayopatikana katika kata husika, hivyo wenyeviti wa vijiji na vitongoji watalipwa asilimia 20 itokanayo na makusanyo ya mapato, hii itasaidia pia kuongeza mapato yetu ya halmashauri, hivyo watendaji wa kata na vijiji wana wajibu wa kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unaongezeka kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya mapato”.
Hivyo baraza limetaka utekelezaji wa malipo hayo kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji ufanyike kwa wakati ili kurahisisha ufanisi wa ufanyaji kazi kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji. Mkurugenzi mtendaji, ameahidi kuendelea kufanyia kazi suala hilo sababu ni moja ya suala linalohitaji muda wa utekelezaji wake.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa