Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhandisi Mohamed Yamlinga amesema posho za wenyeviti wa vijiji na vitongoji wa Wilaya ya Busega tayari zimeanza kulipwa.
Yamlinga ameyasema hayo katika baraza la madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Busega lililofanyika mapema mwishoni mwa wiki hii katika ukumbi wa SILSOS uliopo katika kata ya Nyashimo wilayani hapa. Aliendelea kulieleza baraza kuwa Halmashauri inaendelea kufanya juhudi za kina ili kuhakikisha malimbikizo yote ya posho yanalipwa ndani ya kipindi kifupi.
Naye mhasibu wa mapato ya ndani ya Halmashauri, Bwana Gumuka Misambo, amesisitiza kuwa tayari kiasi cha Shilingi 4,182,000 kwa kata ya Kalemela, Kiloleli, Lamadi,Igalukilo na Nyaluhande kimeishalipwa huku kiasi cha shilingi milioni 40 kimeishalipwa kwa waheshimiwa madiwani kupitia benki ya CRDB. Gumuka ameendelea kulieleza baraza kuwa kumekuwa na changamoto sana wakati wa kuwalipa posho kwani mara nyingi wanakuta akaunti zilizofunguliwa na kata ni ‘dormant’ hivyo kufanya zoezi la ulipaji kuwa gumu.
Aidha, afisa Kilimo wa Wilaya ya Busega Bwana Juma Chacha amesema kuwa pembejeo zilishasambazwa kwa wakulima wa Wilaya hii ingawa baadhi wa wakulima hufanya uzembe na kukaa muda mrefu bila kwenda kuchukua pembejeo hizo na kusababisha uharibifu baada ya kukaa muda mrefu, Bwana Chacha ametoa maelezo hayo baada ya mjumbe wa baraza kutaka kujua kama pembejeo ziishaanza kusambazwa kwa wakulima. Chacha ameshauri wakulima kujitokeza mara moja kuchukua pembejeo mara tu zinapoletwa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera amesisitiza wananchi wote kuwaandikisha watoto wao walio na umri wa chini ya miaka mitano (5) katika vituo vya kusajili watoto ili wapewe vyeti vya kuzaliwa kwani ni haki ya watoto kupata vyeti hivyo.Pia Mhe. Tano amesisitiza vikao vya baraza visichukue siku nzima na badala yake vifuate taratibu, kanuni na sheria zilizowekwa.
Katika Hatua nyingine, Mwakilishi kutoka katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bwana Maganga amewahasa waheshimiwa madiwani wote kuwa na njia mbadala za kuhakikisha kunakuwa na viwanda vidogo vidogo katika kata zao ili kuunga mkono juhudi za Serikali hii ya awamu ya tano ya uanzishwaji na uboreshwaji wa viwanda vya ndani. Maganga amesisitiza kuwa viwanda hivyo vitasaidia kukuza uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa