Waziri wa maliasili na utalii, Dk Hamis Kigwangala, amewataka wananchi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya pori la akiba kijereshi lililoko Wilayani Busega Mkoani Simiyu, ambao wameanzisha makazi na kufanya shughuli za kijamii kwenye eneo la mitaa 500 (buffer zone) kutoka kwenye mpaka wa pori hilo kuondoka mara moja.
Ametoa agizo hilo jana alipotembelea pori hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake kwa ajili ya kukagua shughuli za uhifadhi, baada ya kushuhudia makazi na shughuli nyingine za kibinadamu ndani ya pori hilo kutoa agizo hilo na kusema kuwa sheria za uhifadhi wa wanyamapori haziruhusu vitendo hivyo ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria pamoja na kingo zake (buffer zone) ambazo ni mita 500 kutoka kwenye mpaka halisi wa eneo la hifadhi.
"Mpaka itakapofika tarehe 31 mwezi ujao wananchi wote hawa wawe wameshaondoka eneo hili kwa hiari yao wenyewe, muwatangazie na mpime eneo hili vizuri muweke alama ili wajue ni wapi wanatakiwa kuondoka.
"Na ikifika tarehe 1 Septemba kama kuna watakaokuwa wamekaidi agizo hili, basi mfanye oparesheni maalum muwaondoe na msafishe kila kitu, ni lazima ifike mahali kila mmoja aheshimu sheria za nchi" alisema Dk. Kigwangalla kuuagiza uongozi wa pori hilo.
Wakati huo huo, Waziri Kigwangalla ametoa miezi mitatu kwa mwekezaji wa hoteli ya kitalii ya Kijereshi Tented Camp kurudisha kwa Kamishna wa Ardhi hati miliki ya kipande cha ardhi chenye ukubwa wa hekta 464 kilichopo ndani ya pori hilo kwakuwa ni batili; kwa kuwa pori hilo lilianzishwa mwaka 1994 wakati mwekezaji huyo anadai kumilikishwa eneo hilo mwaka 1995.
Aidha, amemtaka pia mwekezaji huyo kuheshimu sheria na taratibu za uwekezaji katika eneo hilo ikiwemo kulipa ada na tozo mbalimbali.
Awali akimweleza Waziri Meneja wa Pori hilo Diana Chambi alisema kuwa wananchi waliovamia hifadhi ya pori hilo ni kutoka kwenye vijiji vya Lukungu, Mwabayanda, mwakiloba, kijirishi pamoja na Igwata, ambao alieleza waliomba kupewa muda mpaka mwezi Agosti mwaka huu wavune mazao waliyolima ili waondoke kwa hiari kwenye eneo la hifadhi hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe.Tano Mwera, alimuomba waziri kuisaidia idara ya Ardhi na Maliasili ya halmashauri hiyo Gari kwa ajili ya kufanya doria mbalimbali kwenye hifadhi ya pori hilo ili kukabiliana na vitendo vya ujangili pamoja na wanyama kuvamia makazi ya wananchi.
Mara baada ya kutembelea pori hilo, Mhe.Waziri Kigwangala alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ambaye amesema Mkoa huo unafanya juhudi katika kukuza utalii kwa kujenga uwezo wa utamaduni wa ndani na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo ikiwa ni pamoja na Mapori ya Akiba ya Maswa na Kijereshi.
Aidha, Mtaka aliongeza kuwa Serikali imepanga kujenga uwanja wa ndege katika eneo la Igegu wilayani Bariadi ambapo ni jirani kabisa na Hifadhi ya Taifaya Serengeti hivyo itawarahisishia watalii kufikia kwa urahisi hifadhi ya Taifa ya Serengeti kufanya shughuli za Kitalii.
Pori la Akiba Kijereshi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 65.72 linasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA na lilipandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka 1994 kwa Tangazo la Serikali Na. 215 la terehe 10 Juni, 1994 na hiyo ni kutokana na umuhimu wake kiuchumi na kiikolojia hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
MWISHO
Source: www.simiyu.go.tz
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa