Wazazi Wilayani Busega wameaswa kushiriki vyema katika kukuza Elimu kuongeza ufaulu wa wanafunzi wanaohitimu elimu ya Msingi. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria alipokutana na wanafunzi wa Darasa la Saba wanaotarajia kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi. Katika ziara ya kukutana na wanafunzi hao Mhe. Zakaria amesema hakuna budi wazazi kusimama mstari wa mbele katika kuhakikisha Watoto wanapata haki yao ya Elimu.
Aidha, mhe. Zakaria amesema hatowaonea haya wazazi ambao watakatisha masomo Watoto kwasababu mbalimbali ikiwemo kuwaozesha au kuwashughulisha kazi mbalimbali ambazo zitawafanya waaache shule.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore amewataka Wanafunzi wanaotarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi wilayani Busega kuwa makini wanapokuwa katika kipindi hiki kwani umakini husaidia mwanafuznzi kujibu mtihani kwa ufasaha lakini ameomba maandalizi yasiwe kwa darasa la saba tu bali yaanze kwa madarasa ya chini.
Afisa Elimu Wilaya ya Busega Shule za Msingi Bw. Gidion Bunto amesema ni wakati umefika kwa wazazi kushirikiana na walimu ili kutokomeza suala la utoro kwani wapo wanafunzi wengi ambao hutoka nyumbani Kwenda shule lakini huwa hawafiki shuleni. Bw. Bunto amesema wazazi wengi hawajui kama Watoto wao hawahudhurii vipindi mashuleni hivyo ni vyema wazazi washirikiane na walimu ili kujua Maendeleo ya Watoto wao.
Kwa upande wao Wanafunzi wa darasa la saba wanasema kwamba wamejiandaa kufanya mtihani wa kuhitimu shule ya Msingi na wanaamini watafanya vyema kulingana na maandalizi waliyoyapata kutoka kwa walimu.
Wanafunzi wapatao 7,539 wilayani Busega wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi ambapo kati yao wavulana ni 3,598 na wasichana ni 3,941 ukilinganisha na mwaka jana ambapo waliofanya mtihani wa kuhitimu elimu ya Msingi ni wanafunzi 6,562 ambapo wavulana ni 3,158 na wasichana ni 3,404. Mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi unatarajiwa kufanyika tarehe 8 na 9 Septemba 2021.
Mwisho
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa