Watumishi wa Umma wameaswa kuwa na bidii na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Hayo yamesemwa na Afisa Kazi kanda ya Ziwa Bw. Gudlucky Luginga wakati wa Baraza la Wafanyakazi Wilaya ya Busega lililofanyika tarehe 03 Februari 2021 katika Ukumbi wa Silsos, ikiwa ni ufunguzi wa baraza hilo.
Bw. Luginga amewataka wafanyakazi wa umma kukumbuka maadili na wajibu wao ambao unamtaka kila mtumishi wa umma kufanya kazi kwa lengo la kufanikisha malengo ya taasisi husika. Hata hivyo Bw. Luginga ameeleza kwamba uadilifu na bidii ya wafanyakazi inaenda sambamba na mazingira bora ya kazi.
Aidha Bw.Luginga amewataka wajumbe wa baraza hilo kuwa na mawazo chanya ili kulifanya baraza hilo kuwa na maamuzi yanayoenda sambamba na kasi ya maendeleo. “Tunataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi lenye watu wenye mawazo yanayojenga na sio vinginevyo” aliongeza Bw. Luginga.
Awali, Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Busega Bw. Mussa Mmbyana aliendesha uchaguzi wa kumpata Katibu na Katibu Msaidizi wa baraza hilo ambapo wagombea wawili waliopendekezwa waliweza kupigiwa kura. Katika Uchaguzi huo Bw. Elly Msanisa aliweza kuibuka mshindi kwa kupata kura 24 na kutangazwa kuwa Katibu wa baraza hilo, huku Bi. Anna Mkandi aliyeshika nafasi ya pili kwa kupata kura 18 na kutangazwa kuwa Katibu Msaidizi, ambapo watakuwa kwenye nafasi hizo kwa kipindi cha miaka mitatu.
Wajumbe waliohudhuria wamepata fursa ya kuelezwa majukumu ya baraza hilo ikiwemo kuimarisha mipango mbalimbali inayotekelezwa ngazi ya halmashauri na jinsi gani wanatakiwa kuelimisha wafanyakazi juu ya maadili bora katika maeneo yao ya kazi. Aidha, Baraza la Wafanyakazi wilayani Busega limepitia na kuipitisha Mapendekezo ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Kwa upande mwingine, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi Wilaya ya Busega Bw. Msanisa amewashukuru wajumbe wote kwa kumchagua na ameahidi kushirikiana nao katika utekelezaji wa majukumu yote yanayofanywa na baraza hilo. Wajumbe waliohudhuria baraza hilo ni pamoja na viongozi kutoka Chama Cha Walimu (CWT) ngazi ya Mkoa na Wilaya, Chama Cha Wafanyakazi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (TALGWU), Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), Wakuu wa Idara, Vitengo na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa