Watumishi wa Umma Wilayani Busega wametakiwa mara kwa mara kushiriki katika michezo ili kujenga na kuimarisha afya zao. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria wakati wa bonanza la michezo lililofanyika siku ya Jumamosi 19 Machi 2022, ambapo limeshirikisha taasisi za Serikali zilizopo Wilayani Busega.
Zakaria amesema ni vyema Watumishi wakashiriki michezo ili kuimarisha afya, kwani ushiriki katika michezo kwa kiasi kikubwa humfanya mtu kutokuwa na magonjwa ambayo hudhoofisha afya. “Bado mwamko ni mdogo wa ushiriki katika michezo, nimekuwa nikishiriki mazoezi, lakini wanaohudhuria ni wachache sana na wengi wakiwa ni wanafunzi, naomba tushiriki katika michezo kwa wingi ili kuimarisha afya zetu”. Aliongeza Zakaria.
Kwa upande mwingine Zakaria amesema kupitia michezo mbalimbali ikiwemo ya dansi, vijana wengi wanaweza kujiajiri na kujipatia kipato kikubwa kama ilivyo kwa baadhi ya wasanii wakubwa waliopo nchini. “Mimi ni mdau mzuri wa michezo, na nipo tayari kuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunakuwa na michezo mbalimbali Wilayani kwetu ili kutengeneza ajira kwa vijana wetu, kwani licha ya michezo kusaidia kuimarisha afya lakini pia hutengeneza ajira”, alisema Zakaria.
Washindi wa michezo mbalimbali walipatiwa zawadi ambapo kwa upande wa mpira wa miguu wanaume, timu ya Polisi Busega ilifanikiwa kuwa mshindi wa kwanza baada ya kuifunga timu ya Halmashauri Makao Makuu katika mchezo wa fainali kwa mikwaju ya penati 5-4, upande wa netiboli timu ya walimu iliibuka kidedea baada ya kuifunga timu ya Halmashauri Makao Makuu. Kwa upande wa riadha wanaume mita 100 mshindi ni Mohamed Rashid ambaye ni Mwalimu, mita 100 wanawake mshindi ni Piencia Mgizi ambae pia ni Mwalimu. Washindi wa nafasi ya kwanza hadi nafasi ya tatu kwa upande wa riadha na kukimbia kinyumenyume wamepatiwa fedha taslimu.Kwa mchezo wa kukimbia kinyumenyume mita 100 upande wa wanaume mshindi ni Betram Mwanga ambae ni Polisi, upande wa wanawake mshindi ni Piencia Mgizi ambae ni Mwalimu. Bonanza hilo linafanyika ikiwa na lengo la kuwaleta pamoja Watumishi wa Umma kwaajili ya kubadilishana mawazo, uzoefu na ujuzi mbalimbali.
Taasisi zilizoshiriki ni pamoja na timu ya Watumishi wa Halmashauri Makao Makuu Walimu Msingi, Walimu Sekondari, Watumishi Idara ya Afya, huku taasisi zinginezo zilizoshiriki ni TANESCO na Polisi, huku kila timu ikipata zawadi ya kondoo mmoja na pesa taslimu kwa mshindi wa kwanza na wa pili kwa upande wa mpira wa miguu. Washiriki wanasema kufanyika kwa bonanza hilo ni jambo jema na la Msingi, lakini wameomba viongozi na wadau kuwezesha bonanza hilo ili kuwa na ubora zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa