Watu watano wamejeruhiwa na Chui katika kijiji cha Shimanihirwe, kata ya Kabita wilayani Busega, mnamo tarehe 23/03/2020. Katika mkasa huo uliowaacha wananchi wakiwa na hofu uliweza kuhitimishwa na Kikosi Dhidi ya Ujangili (KDU) Kanda ya Serengeti kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Busega majira ya jioni.
Kwa mujibu wa Afisa Wanyama pori kutoka kikosi hicho, John Msirikale, amedai kwamba Chui huyo inawezekana ametoroka kutoka Mbuga ya Wanyama ya Serengeti na kuingia kwenye kijiji hicho ambapo alileta taharuki ya kushambulia wananchi, na sababu kubwa ikiwa ni kuzongwa na baadhi ya wanakijiji. “Kazi yetu sio kudhuru wanyama, bali kuwalinda na kuwaongoza warejee mbugani, lakini ikitokea mnyama ameleta madhara na anaendelea kuleta madhara huwa tunachukua hatua ya kumuua ili kuokoa maisha ya wananchi, hicho ndicho tulichokifanya” alisema Msirikale.
Katika taharuki hiyo jumla ya watu watano wamejeruhiwa na wameweza kupatiwa huduma na mmoja kati yao amelazwa kituo cha Afya Nassa kwa matibabu zaidi kutokana na majeraha aliyoweza kuyapata kwa kushambuliwa na Chui huyo. Hali ya mgonjwa huyo ambae alionekana kuwa na majeraha maeneo ya tumbo inaendelea vizuri na anaendelea kupata matibabu.
Mashuhuda wanasema Chui huyo alikuwa akionekana kijijini hapo kwa muda mrefu kwa siku hiyo ya tukio na kuwa na hatari kubwa hasa kwa watoto na wazee. Wameishukuru ofisi ya mkurugenzi mtendaji kwa bidii iliyooneshwa kwa kudhibiti hali hiyo na kuweza kumuua Chui huyo ambae alionekana tishio katika kijiji hicho.
Visa vya wanyama pori kuingia kwenye makazi ya wananchi imekua ikijitokeza mara kwa mara kwenye vijiji vingi wilayani Busega hasa vile vilivyopo pembezoni mwa ziwa Victoria na vilivyopakana na Mbuga ya Serengeti. Hivyo wananchi wanaaswa kuwa makini na wanyama wanapoingia kwenye makazi yao kwa kuhakikisha wanakaa mbali nao na kutoa taarifa ya haraka kwa vyombo vinavyohusika.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa