Ziara ya siku moja ya Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ya kutembelea kampuni zinazohusika na uozeshaji wa marudio ya mchanga wa dhahabu (Plant) iliyofanyika tarehe 19 Novemba 2021, imelenga kupata picha ya hali halisis ya ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri. Katika ziara hiyo Mhe. Zakaria ameweza kuambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Busega, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega na baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega imeweza kubaini upotevu wa mapato ambayo yanatokana na vifusi vya mchanga maarufu kama makinikia.
Mhe. Zakaria amesema kwamba mchanga wote unaoletwa maeneo ambayo yanatumika kuozesha marudio ya mchanga wa dhahabu ni lazima ulipiwe ushuru wa Halmashauri kwani ndio utaratibu. Pamoja na hayo Mhe. Zakaria amesema kwamba kuna umuhimu kukutana na wamiliki wa kampuni hizo ili kuongea lugha moja kabla ya utekelezaji wake kuanza, huku akimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kuhakikisha anapeleka wataalam kwenye kampuni zote zinazofanya shughuli hiyo ili kutathmini thamani ya vifusi vilivyopo kwaajili ya kulipiwa ushuru.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore amesema kuna umuhimu kwa wamiliki wa kampuni hizo kushirikiana kwa ukaribu na Ofisi ya Halmashauri ili kuhakikisha makampuni hayo yanaendesha shughuli zao bila vikwazo. “Shughuli hizo mnazozifanya ni halali lakini uhalali wake unathibitisha na kufauata vigezo na taratibu za Serikali ikiwemo kulipa ushuru”, aliongeza Sayore.
Kwa upande mwingine Mhe. Zakaria ameweza kutembelea mgodi wa dhahabu wa Imalalamate na kujionea shughuli mbalimbali zikiendelea huku akisisitiza udhibiti wa mifuko ya mchanga siku za minada. Zakaria amesema kwamba ni vyema viroba vya mchanga vikawekwa sehemu moja siku ya mnada ili kudhibiti utoroshwaji wa viroba hivyo kwa lengo la kudhibiti upotevu wa mapato ya Halmashauri. Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega inaendelea kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha makusanyo ya mapato ya ndani yanaendelea kupanda ili kufikia malengo ya bajeti ya Halmashauri.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa