Wananchi watakiwa kushiriki kikamilifu katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali. Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera wakati wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Busega ilipotembelea miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na serikali wilayani Busega.
Mhe. Tano Mwera amewataka wananchi kuwa na mwamko katika miradi mbalimbali inayoletwa na serikali wilayani Busega, kwani kufanya hivyo ni dhahiri kwamba wananchi wamependezwa na ujio wa maendeleo wilayani Busega. Amewataka mwananchi wasimame katika nafasi zao ili kuhakikisha miradi inasimama na kumalizika kwa wakati.
Mhe. Mwera amesisitiza kama wananchi wanatakiwa kushiriki kupitia nguvu kazi basi washiriki ipasavyo, na kama watatakiwa kuchangia basi pia wafanye hivyo kwa miradi inayohitaji ushiriki wao. Aidha amewaomba viongozi ngazi ya vijiji kuhamasisha wananchi kushirki miradi mbalimbali kwani miradi hiyo imeletwa kwaajili yao hivyo hawana budi kuipokea kwa mikono miwili hii itachangia serikali kutaka kuleta miradi mingi Zaidi.
Katika ziara hiyo miradi mbalimbali ilitembelewa ikiwemo ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Busega, ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari, ujenzi wa majengo kwenye zahanati, ujenzi wa nyumba za watumishi na ujenzi wa miundombinu kwenye Hospitali ya Wilaya ya Busega huku kamati ya ulinzi na usalama ikiridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Anderson N. Kabuko ameongeza kwamba miradi ambayo imetekelezwa ni juhudi za watendaji ambao wamekuwa na utendaji mzuri matokeo yake ni kukamilika kwa wakati miradi mbalimbali, lakini pia amesisitiza miradi inayoendelea na utekelezaji wake itakamilika kwa muda uliopangwa.
Wilaya ya Busega imetekeleza na inaendelea na utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo ili kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi. Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Busega wanafurahishwa na kasi ya maendeleo na kuomba serikali kuleta miradi mingi zaidi ili maendeleo yawe ya haraka zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa