Wakulima wa zao la Pamba Wilayani Busega wameanza kupatiwa elimu ya upuliziaji dawa katika mashamba yao ili kuondoa wadudu waharibifu wa zao hilo. Katika mafunzo hayo ya siku tatu kuanzia tarehe 07-09 Machi, 2022 yanajumuisha wakulima wa zao hilo katika Kata zote 15 zilizopo Wilayani Busega.
Balozi wa zao la Pamba nchini Bw. Aggrey Mwanri akiambata na mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria wameweza kukutana na wakulima katika maeneo yao ili kutoa elimu ya moja kwa moja kwa vitendo. Katika Mafunzo hayo wakulima wanaelimishwa namna bora ya uchanganyaji wa dawa na upuliziaji unaostahili ili kudhibiti wadudu waharibifu.
“Lengo la kuja kukutana na wakulima katika mashamba yao ni kuonesha namna ya uchanganyaji na upuliziaji wa dawa katika shamba ili kudhibiti wadudu waharibifu wakiwemo funza na chawa jani”, alisema Mwanri. Aidha, Mwanri amesema ili kuwa na tija ya zao la Pamba ni vyema wakulima kupatiwa elimu ya mara kwa mara ya jinsi ya uchanganyaji wa dawa na upuliziaji kwani juhudi za wakulima zitarudishwa nyuma pale tu udhibiti wa wadudu utapuuziwa.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amewataka wakulima kufuata maelekezo ya wataalam ili kuwa na uzalishaji wenye tija wa zao hilo kuliko kulima kwa mazoea kama ilivyo hapo awali. “Tujiatahidi kufuata maelekezo ya wataam ili kuongeza uzalishaji wa Pamba na kufikia lengo la Wilaya la kuzaliza tani 50,000 kwa msimu wa mwaka huu, tulime kwa kufuata vipimo vya wataalam kama ilivyoelekezwa kwamba ni umbali wa sentimeta 60-30 kutoka shina moja hadi lingine, alisema Zakaria.
Pamoja na hayo, Zakaria ameweza kuwapatia mabomba ya kupulizia dawa wakulima ambao wamefanya vizuri zaidi kwa lengo la kuwaongezea motisha zaidi, huku akitoa tahadhari kwa wote ambao watagawa dawa hizo bila kuzangatia miongozo na taratibu. Nao wakulima wa Pamba wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita na kumshukuru Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mhe. Samia suluhu Hassan kwa hatua anazoendelea kuzifanya ikiwemo utoaji wa mkopo wa viuatilifu kwa wakulima kwa lengo la kuhakikisha wakulima wanapata uzalishaji wenye tija kubwa.
Mwisho
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa