Mradi wa kilimo cha kisasa cha mpunga Wilayani Busega una lengo la kuwawezesha wakulima waweze kuingia kwenye kilimo cha biashara. Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Busega Mazao Limited, Bw. Deogratius Kumalija wakati wa kikao kilichofanyika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega tarehe 11 Septemba, 2020.
Kampuni ya Busega Mazao inatarajia kutekeleza mradi wa Kilimo cha Kisasa cha Mpunga unaojulikana kama Competitive African Rice Initiative-East Africa (CARI-EA) Wilayani Busega. Bw. Kumalija amesema kwamba mradi huo utaanza kutekelezwa katika vijiji zaidi ya tisa ikiwemo Mwanangi, Busami, Sanga, Mwamgoba, Nyangoko, Jisesa na Shigala, kwa wakulima kuwezeshwa mbegu za kisasa, utumiaji wa teknolojia bora ya upandaji, upaliliaji wa kisasa na upatikanaji wa soko la uhakika, huku amesisitiza kwamba wameanza na vijiji vichache lakini kwa hapo baadae vijiji vingine zaidi vitaingizwa kwenye mradi huo.
Kampuni ya Busega Mazao Limited kwa kushikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Busega itafanya kazi na wakulima wapatao 10,000 wa kilimo cha mpunga, kwa kuwapa mbinu bora na za kisasa za kilimo ili kuweza kufikia malengo ya wakulima wa Mpunga Wilayani Busega, aliongeza Bw. Kumalija.
Awali Mratibu wa Mradi Bw. Innocent Mafuru ameeleza kwamba kabla ya kutekelezwa kwa mradi huo wakulima wote watakaoingia kwenye mradi huo watapatiwa mafunzo ili kuwawezesha kuwa na uelewa wa mradi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Anderson Njiginya Kabuko ameipongeza kampuni ya Busega Mazao kwa mradi huo na kukiri kwamba ni heshima kubwa kwa Wilaya ya Busega hivyo ni wajibu wa Ofisi ya Mkurugenzi kushiriki kikamilifu katika mradi huo. Tunashukuru kwa kutushirikisha na kiukweli mmetupa heshima kubwa hivyo tunatoa pongezi nyingi kwa uongozi wa kampuni ya Busega Mazao na naahidi tutashirikiana nanyi vyema ili kufikia lengo la mradi, aliongeza Kabuko.
Aidha, Kabuko ameiomba kampuni hiyo kutenga eneo maalumu litakalotumika kwa kilimo ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo kuwa na ufanisi mkubwa. Kikao hicho kikihudhuriwa pia na Afisa Kilimo na Ushirika, Bw. Juma Chacha na baadhi ya wataalamu wengine kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa