Kikao cha wadau wa uchaguzi kimefanyika siku ya tarehe 20/08/2020 wilayani Busega, huku wadau wakitakiwa kushiriki kikamilifu ili kufanikisha uchaguzi mkuu oktoba 2020.
Kikao hicho kilichowakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo vyama vya siasa, kamati ya ulinzi na usalama, makundi ya walemavu, makundi ya wazee, makundi ya wafanyabiashara, viongozi wa dini, makundi ya wanawake, makundi ya vijana na wataalam wa kada tofauti kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Busega, kilikuwa kikao chenye manufaa makubwa kwa wadau wote kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera amewataka wadau wote kusimama kwenye nafasi zao ili kwa pamoja uchaguzi ufanyike kwa kufuata kanuni na taratibu zilizoelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuomba vyama vyote vitakavyoshiriki uchaguzi kujinadi kwa sera safi na sio vinginevyo. Amesisitiza kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki kwani anatambua uwepo wa demokrasia iliyopo nchini. Utakapofika muda wa kufanya kampeni tujitahidi kutumia lugha zenye staha, tuache lugha za kejeli na lugha za matusi kwani zitasababisha chuki, aliongeza Mhe. Mwera.
Kwa upande mwingine Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Busega, Anderson Njiginya Kabuko amewaomba wadau hao kushirkiana vyema kwa kila hatua ili kufanikisha uchaguzi. Viongozi wa dini nyie ni chachu kubwa ya kufanikisha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hivyo naomba msimame katika nafasi yenu hasa kwa kuliombea taifa ili mchakato wote wa uchaguzi uweze kwenda vizuri, alisema Kabuko.
Wadau hao pia wameweza kukumbushwa maadili mbalimbali katika kipindi cha uchaguzi, ikiwemo kutojihusisha na vitendo vya rushwa. Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Hamad Mabula amewaomba wadau wote kutojihusisha na vitendo vya rushwa na kusisitiza kwamba serikali haitasita kuwachukulia hatua wote watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi. Rushwa ina madhara makubwa sana kwenye uchaguzi kwani huweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuvuruga zoezi la uchaguzi hivyo huweza kuisababishia serikali gharama zisizo za lazima, aliongeza Bw. Mabula.
Kwa upande wa wadau waliohudhuria kikao hicho wamekiri kwamba kikao hicho kimewaonesha dira kubwa kuelekea uchaguzi mkuu oktoba 2020. Wametoa shukrani zao kwa Mkuu wa Wilaya na Msimamizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kwa pamoja kufanikisha kikao hicho muhimu na kupongeza mchakato wa uchaguzi unavyoendelea jimbo la Busega.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa