Uongozi wa Wilaya ya Busega umewataka wadau wa maendeleo na wazawa wa Wilaya ya Busega kushiriki vyema katika maendeleo. Hayo yamesemwa wakati wa harambee ya kuchangia ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu inayopungua katika Shule za Sekondari iliyofanyika siku ya Jumamosi tarehe 02 Oktoba 2021.
Mgeni rasmi katika harambee hiyo alikuwa Mhe. Gabriel Zakaria Mkuu wa Wilaya ya Busega akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Simiyu. Harambee hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, ikiwemo taasisi za Serikali na binafsi, viongozi wa Serikali ngazi mbalimbali, viongozi wa dini na watumishi wa Wilaya ya Busega.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema Wilaya itahakikisha inaelekeza fedha zote za harambee hiyo kwenye ukamilishaji wa miundombinu katika shule za Sekondari, ili kutimiza lengo la harambee hiyo. Aidha, Mhe. Zakaria amesema wadau wanayo nafasi kubwa kushiriki katika maendeleo, kwani Serikali inatambua mchango wao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bi. Veronica Sayore amesema ni muhimu kwa uongozi wa Wilaya kuendelea na ushirikiano ili kuhakikisha changamoto ya miundombinu ya madarasa katika mashule inapatiwa ufumbuzi. Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa za kutengeneza mazingira bora kwenye Sekta ya Elimu.
Wadau walioshiriki harambee hiyo wameupongeza Uongozi wa Wilaya ya Busega kwa hatua hiyo na kusema kwamba kwa umoja wao kama wadau wapo tayari kushirikiana na Serikali katika maendeleo ya Wilaya ya Busega. Wilaya ya Busega ina upungufu wa vyumba vya madarasa vipatavyo 79 katika shule za Sekondari, huku idadi ya wanafunzi 6442 wanatarajiwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2022, hivyo kupelekea jumla ya wanafunzi kufikia 16,631 kutoka wanafunzi 13,933 waliopo sasa katika shule za Sekondari.
Mwisho
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa