Maonesho ya wakulima, Nananane mwaka 2020 yamefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 01/08/2020, ikiwa ni mwaka wa tatu mfululizo Kitaifa kufanyika Mkoa wa Simiyu.
Ushiriki wa halmashauri ya Busega umekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi mbalimbali wanaotembelea maonesho hayo. Kwa mwaka huu 2020 halmashauri ya wilaya ya Busega imekuwa na ubunifu katika kilimo, uvuvi, ufugaji na ujasiriamali.
KILIMO
Kilimo ni moja ya shughuli kubwa zinazofanywa wilayani Busega hivyo katika maonesho ya mwaka huu halmashauri imeweza kuandaa elimu ya shamba darasa.
Bustani za Nyumbani; kilimo cha bustani ni changamoto kwa wakulima wengi hivyo umuhimu wa kilimo hiki ni muhimu sababu huinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na kwa haraka. Bustani za nyumbani hujumuisha kilimo cha mbogamboga spinach, kabeji, mchicha na Vitunguu.
Kilimo cha Mpunga; kilimo cha mpunga ni miongoni mwa kilimo kinacholimwa kwa wingi nchini hivyo halmashauri ya wilaya ya Busega inaonesha na kutoa elimu ya kilimo cha mpunga. Elimu ya kulima wakati wa masika na kiangazi ambapo kilimo cha umwagiliaji huchukua nafasi Zaidi.
Kilimo cha Matikiti; kilimo hiki ni miongoni mwa kilimo cha biashara kinacholimwa sehemu mbalimbali nchini hivyo halmashauri ya wilaya ya Busega kupitia idara ya Kilimo na Ushirika pia imeweza kuonesha na kutoa elimu ya kilimo cha matikiti aina ya Kito.
Kilimo cha Vitunguu Vyekundu; elimu na ushauri ya kilimo cha vitunguu vyekundu pia inatolewa kwa wakulima ili kuchochea teknolojia bora ya kilimo cha vitunguu hasa vitunguu vyekundu.
Kilimo cha Nyanya; kilimo cha nyanya ni moja ya kilimo kinachohitaji elimu ya uzalishaji wake hivyo mkulima hana budi kupata elimu ya wataalam wa kilimo ili kuweza kulima kisasa kwa kufuata teknolojia ya kilimo hicho.
Kilimo cha Matango; kilimo cha matango kinahitaji maelekezo ya wataam wa kilimo kama ilivyo kwa kilimo cha mazao mengine. Hivyo halmashauri ya wilaya ya Busega imeona hilo ni jambo muhimu na kutoa fursa kwa wakulima kupata elimu ya kilimo cha zao hilo.
Kilimo cha Pamba; kilimo cha pamba ni moja ya kilimo kinacholimwa kwa wingi mkoani Simiyu na kanda ya ziwa kwa ujumla. Ni moja ya zao la biashara linaloingiza pato kubwa nchini hivyo kilimo chake kinahitaji ushauri na maelekezo ya wataalam wa kilimo. Halmashauri ya wilaya ya Busega inatoa elimu, ushauri na maelekezo ya kitaalam kuhusu kilimo cha Pamba.
Kilimo cha Mtama; kilimo cha mtama ni moja ya zao linalolimwa sehemu mbalimbali nchini na moja ya kilimo kinachohitaji ushauri wa kulima kwa wakati hivyo elimu na ushauri unahitaji maelekezo ya kitaalam ili kufanikiwa kuzalisha kwa wingi.
Kilimo cha Mahindi na Ufuta; kilimo cha mahindi na ufuta ni muhimu kupata maelekezo ya kitaalam. Wakulima wengi wamekuwa wakilima kwa mazoea hivyo kufanya kilimo cha mahindi na ufuta kudumaa.
Mtaalma wa Kilimo kutoka halmashauri ya wilaya ya Busega ameeleza kwamba wakulima wanatakiwa kutumia dawa asilia ikiwemo Ndulele na Masangusangu kwaajili ya kuua wadudu haribifu wanaoharibu mazao. Dawa hizi ni mbadala wa dawa zinazotengenezwa viwandani na hazina kemikali zinazoweza sababisha madhara kwa mazao.
VIKUNDI VYA MAENDELEO
Ushiriki wa vikundi vya wajasiriamali kutoka Busega katika maonesho ya Nanenane mwaka 2020 umekuwa na ubunifu wa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali. Miongoni mwa vikundi hivyo ni vile vinavyofaidika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na halmashauri ya wilaya ya Busega ni kama ifuatavyo;
Simiyu Shoes Product; Hiki ni kikundi kinachopatikana wilayani Busega kinazalisha na kutengeneza Viatu. Utengenezaji wa viatu kwa kutumia Ngozi hufanywa na kikundi hicho na kuweza kuwa na mtazamo wa Tanzania ya Viwanda.
Wanawake Faraja; ni kikundi cha akina mama kutoka wilayani Busega ambacho kinajihusisha na utengenezaji wa mikoba asili ya akina mama na urembo ambao huendana na utamaduni wa Mtanzania.
Maua School of Designing and Arts; kikundi hiki kinajihusisha kutoa mafunzo ya ushonaji wa nguo mbalimbali, upambaji na utengenezaji wa urembo aina mbalimbali. Ni kikundi kinachopatikana wilayani Busega pia hushiriki maonesho ya Nanenane ikiwemo maonesho ya mwaka huu 2020.
Kikundi cha Umoja ni Nguvu; ni kikundi kinachojihusisha na uchakataji wa samaki. Samaki hupatikana kwa wingi wilayani Busega ikiwemo Sangara na Sato, hivyo kikundi cha Umoja ni Nguvu huchakata samaki hivyo kufanya soko la samaki kuongezeka.
KiOM Milk; ni kikundi cha ujasiriamali kinachojihusisha na usindikaji wa Maziwa. Ni miongoni mwa kikundi kinachoshiriki maonesho ya Nanenane 2020.
MIFUGO NA UVUVI
Idara ya Mifugo na Uvuvi kutoka halmashauri ya wilaya ya Busega imeshiriki katika maonesho ya Nanenane 2020 kama ilivyo miaka mingine. Katika maonesho ya mwaka huu idara imeweza kuonesha ufugaji wa kisasa wa Ng’ombe, Kuku na Samaki, na kutoa elimu ya njia ya kisasa ya kulisha mifugo.
Ufugaji wa samaki uliounganishwa na banda la kuku, maonesho ya zana za uvuvi ikiwemo mitumbwi na nyavu zinazokubalika kwaajili ya uvuvi maeneo mbalimbali nchini, Uchakataji wa samaki kwa njia ya majiko yaliyotengenezwa kwa tofali na chuma ni elimu inayotolewa na wataalam wa mifugo na uvuvi kutoka halmashauri ya wilaya ya Busega .
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa