Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wa kunusuru kaya masikini, TASAF umekua nuru ya kukomboa kiuchumi kaya masikini Wilayani Busega. Mpango huu ulianza rasmi kwa kaya masikini kutambulika na ugawaji fedha kwa walengwa mwaka 2015 katika wilaya ya Busega. Jumla ya walengwa 3826 wamefaidika na mradi wa TASAF kipindi cha kwanza awamu ya tatu.
Jumla ya vijiji 41 kati ya 59 vimejumuishwa kwenye mpango wa TASAF kipindi cha kwanza awamu ya tatu na zaidi ya Tshs. Milioni 766 ziligaiwa kwa kaya lengwa. Mpango wa TASAF ni miongoni mwa dhima kubwa na kipaumbele cha kupunguza umasikini kwa kaya masikini nchini Tanzania, hivyo serikali na kaya lengwa zina matumanini makubwa katika mpango huu.
Kuwepo kwenye mpango wa TASAF kwa wilaya ya Busega tangu mwaka 2015 ni ushahidi tosha kuwa mpango huu umekuwa mkombozi wa jamii nyingi masikini wilayani humo. Kaya nyingi zimepata mwangaza wa kujikomboa kutoka kwenye dimbwi la umasikini uliopitiliza kwa kujiwekea malengo fanisi ya matumizi ya pesa wanazopata kwa kuwekeza kwenye shughuli za maendeleo.
Shughuli zenye tija na zenye kuchochea maendeleo zinazofanywa na kaya zinazofaidika na mpango wa TASAF kwa wilaya ya Busega ni pamoja na ufugaji, biashara ndogondogo, kusomesha watoto na shughuli za kilimo. Baadhi ya wafaidika wamekiri kwamba mpango huu wa TASAF ni mkombozi kwao kwakua umefanya maisha ya kaya nyingi kuinuka kiuchumi kwa kujishughulisha na ujasirilimali.
Mratibu wa mpango wa TASAF wilaya ya Busega Bi. Wema Mmari amekiri kuwa kuna mwamko mkubwa kwa kaya lengwa kwani zimekuwa katika maendeleo ya kiuchumi kwa kuzingatia malengo bora ya matumizi ya fedha wanazopokea. Kata zote 15 zilizopo wilayani Busega zimekuwa katika mpango wa TASAF awamu ya tatu kipindi cha kwanza. Jamii na kaya lengwa zimekuwa zikipata elimu ya kuhakikisha maisha yao yanaboreshwa kutoka katika utegemezi kwa kutumia fedha wanazopata kikamilifu kwa mambo yenye tija ya ushawishi wa maendeleo. Mpango huu wa kunusuru kaya masikini ni chachu ya maendeleo na mafanikio yake tangu ulipoanza umekuwa ni mkubwa sana.
Kwa kuzingatia umuhimu wa mpango huu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Joseph Maguful, amezindua mpango wa kipindi cha pili cha awamu ya tatu wa kunusuru kaya masikini mapema mwaka huu. Mpango ambao unatarajia kugharimu tirioni 2 za kitanzania kwaajili ya kutoa ruzuku kwa kaya masikini nchni.
Tangu kuanzishwa kwa TASAF nchini Tanzania mwaka 2000 kumekuwa na tija ya kupambana na umaskini kwa kiasi kikubwa maeneo mbalimbali nchini. Hivyo mpango huu ni nuru ya maendeleo kwa nchi nyingi zilizopo kwenye maendeleo ya uchumi wa kati ikiwemo Tanzania. Wachambuzi wa masuala ya kiuchumi wana matumaini kwamba endapo mpango wa kunusuru kaya masikini utaongeza kiwango cha ruzuku katika kaya, utasaidia Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo 2030.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa