Kutokana na kuripotiwa kwa baadhi ya watu nchini walioambukizwa Virusi vya COVID 19, virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona ambao unasambaa kwa kasi duniani, viongozi wa wilaya ya Busega wamechukua tahadhari kwa kukutana na wadau mbalimbali kutoa elimu na tahadhari juu ya ugonjwa huo.
Kikao kilichofanyika tarehe 24/03/2020 katika Hospitali ya Wilaya imejumuisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa juu wa Wilaya, Watendaji, Vyombo vya ulinzi na usalama, Viongozi wa Dini na wadau wengine. Lengo likiwa kutoa elimu elekezi, ufahamu wa kitaalam na hatua za kujikinga na ugonjwa huo.
Katika kikao hicho ambacho kilikuwa kimeangalia ugonjwa wa Corona kitaalam zaidi na kutolewa ufafanuzi wa ugonjwa huo na Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt. Godfrey Mbangali kwa kusisitiza wananchi wasikie mwongozo wa serikali na taarifa rasmi ambazo zinatolewa na vyanzo sahihi, na kuomba kutoa taarifa ya haraka kwa mtu anayehisiwa kuwa na maambukizi ya Corona ili taratibu za vipimo zifanyike kutambua hali ya mshukiwa. “kuchukua tahadhari zilizoainishwa ni muhimu zaidi lakini kusiwe na upotoshwaji wa aina yoyote ambao utasababisha madhara kwa wananchi” alisema Dkt. Mbangali.
Mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe. Tano Mwera ameomba wananchi kuwa makini na taarifa nyingi zinazotelewa na watu wasio na uelewa kuhusu ugonjwa huo na kukemea vikali watu wanaoleta masihara na ugonjwa huo waache mara moja kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria, na pia kukataza mikusanyiko yoyote bila kuwa na sababu zisizo za lazima. Aidha amewaomba wadau kutumia kikao hicho kama tija ya kusambaza elimu sahihi kwa makundi ya jamii zao. “kwakua tuna viongozi wa dini na wadau wengine hivyo ni imani yangu kutakuwa na wigo mpana tukitoka hapa kuelimisha watu wetu juu ya ugonjwa huu, lakini elimu sahihi juu ya tahadhari ya kujikingana dhidi ya ugonjwa huu na sio vinginevyo” aliongeza Mhe. Mwera.
Hatua hizo wilayani Busega zinachukuliwa huku serikali ikiwa imechukua tahadhari kubwa juu ya ugonjwa huo, ikiwemo kufunga shule zote kuanzia awali mpaka elimu ya juu kwa nchi nzima kwa muda wa siku 30 kuanzia tarehe 17/03/2020, kukataza mikusanyiko yoyote isiyo ya lazima na kuhakikisha watu wanafuata taratibu sahihi za kujikinga na virusi aina ya COVID 19 ikiwemo kujali usafi na maelekezo mengine sahihi.
Wadau wanaaswa kuwa mstari wa mbele kuelimisha wananchi juu ya tahadhari sahihi ili kuzuia imani potofu kwa makundi mbalimbali katika jamii juu ya ugonjwa huo, lengo likiwa kuzuia maambukizi kwakua umekuwa ukienea kwa haraka zaidi katika nchi nyingi duniani na kuleta athari ya vifo kwa baadhi ya walioambukizwa na virusi hivyo vya COVID 19.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa