Mbio za Serengeti Safari Marathon ni njia mpya ya kutangaza Utalii katika Hifadhi ya Taifa Serengeti. Hayo yamesemwa na mgeni rasmi Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye kilele cha mbio za Serengeti Safari Marathon zilizofanyika tarehe 14/11/2020. Awali Dkt. Kikwete amesema kwamba Washiriki wa mbio hizo ni Mabalozi wazuri wa kuvutia Utalii wa Hifadhi hiyo, huku akiwapongeza waandaaji wa mbio hizo na kuwataka wazidi kuziboresha ili ziweze kuwa za Kimataifa.
Pia Dr. Kikwete ametaka kutunzwa kwa Hifandi hii ili kuzuia uharibifu na upotevu wa Wanyama. “Hifadhi za Wanyama zilindwe na kutunzwa kama tukitaka hawa Wanyama waendelee kuwepo, tuzuie uchungaji wa Mifugo maeneo ya Hifadhi na kupambana na ujangili ambao miaka ya nyuma ulikuwa tatizo lakini kwa sasa umepungua, hivyo naipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi na hatua zinazofanywa kulinda Hifadhi zetu”, aliongeza Dkt. Kikwete.
Kwa upande mwingine rais wa Chama Cha Riadha Tanzania ambae pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka amesema kuwa mbio za Serengeti Safari Marathon zina mabadiliko makubwa tangu zilipoanzishwa na matarajio ni kuzitangaza zaidi ili ziweze kuwa za Kimataifa kama zilivyo mbio zingine, lengo likiwa ni kuongeza Utalii.
Mbio za Serengeti Safari Marathon mwaka 2020 ni za tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018. Mbio hizi kwa mwaka huu zimehusisha Mikoa miwili, ambapo kwa upande wa Mkoa wa Simiyu ni Wilaya ya Busega na kwa upande wa Mkoa wa Mara ni Wilaya ya Bunda, huku zikianzia na kumalizikia Ndabaka lango kuu la kuingilia Hifadhi hiyo. Mbio hizo zilizokuwa na umbali tofauti wa kuanzia Kilomita 5, Kilomita 10, Kilomita 21 na Kilomita 42, zimeweza kuhusisha Washiriki mbalimbali wa ndani na nje ya nchi huku Watanzania na Wakenya waking’ara katika nafasi za juu.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa