Kilele cha maadhimisho ya 28 ya wakulima, wavuvi na wafugaji, Nanenane yaliyofanyika kitaifa Mkoa wa Simiyu yamehitimishwa tarehe 08/08/2020. Mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amezitaka sekta za kibiashara nchini kuratibiwa vyema ili kuweza kupata masoko ya uhakika kwa wakulima, wavuvi na wafugaji.
Maonesho ya wakulima, wavuvi na wafugaji hufanyika kila mwaka kuanzia tarehe 1 hadi 8 ya mwezi wa nane ili kutoa fursa kwa sekta hii kuweza kupata mafunzo, hamasa na fursa mbalimbali katika maendeleo ya kilimo, uvuvi na ufugaji nchini.
Mhe. Majaliwa amesema sekta ya kilimo ni muhimu nchini kwa maendeleo ya uchumi, kwani huondoa umskini na kukuza ajira nchini. Hivyo amezitaka taasisi za kibiashara nchini zikiwemo wizara zote zinazohusika na mambo ya biashara, taasisi zingine za umma na zisizo za umma kusimama pamoja ili kuweza kukuza na kufanikisha soko la uhakika katika sekta ya kilimo, ikiwemo kuwa na viwanda vya ndani ili kufanikisha uzalishaji wa ndani. Mhe. Majaliwa amesema hayo huku masoko ya uhakika katika sekta hii ikiwa ni moja ya changamoto hivyo huwafanya kudumaa katika uzalishaji.
Aidha Mhe. Majaliwa ameagiza kusimamiwa vyema vyama vya ushirika ili kuleta uhakika wa masoko kwa wakulima katika maeneo yao. Amewataka wakulima wakiwemo wakulima wa pamba nchini kujiunga na vyama vya ushirika kwani vina manufaa makubwa kwao. Tuendelee kusimamia ushirika kama kuna viongozi wanataka kufaidika kupitia ushirika wajiuzulu mapema, tunaendelea kuimarisha ushirika ili kupata masoko ya uhakika kwa wakulima, aliongeza Mhe. Majaliwa.
Mbali na kuzitaka taasisi za kibiashara kuwa imara, pia Mhe. Majaliwa ameagiza kutengwa kwa maeneo maalum katika ngazi za halmashauri kwaajili ya wajasiriamali kufanya biashara zao kwani muda mwingine wanapata shida maeneo ya kufanyia shughuli zao. Kutengewa kwa maeneo kwa wajasiriamali kutawawezesha kuwa na soko la uhakika katika maeneo yao hivyo kuzuia hamahama ya wajasiriamali. Sambamba na hilo Mhe. Majaliwa ameagiza pia halmashauri kubainisha maeneo ya ufugaji ili kuzuia migogoro ya muda mrefu baina ya wakulima na wafugaji nchini.
Katika maonesho hayo, pia uvuvi umeweza kuwa na teknolojia ya kisasa hivyo Mhe. Majaliwa amewataka wavuvi na wadau nchini kuwezesha na kuendeleza ubunifu unaofanywa na wananchi mbalimbali katika uvuvi. Teknolojia ya kisasa ya ufugaji wa samaki ni miongoni mwa mambo muhimu ya kuzingatiwa katika uvuvi na kuzitaka halmashauri kutumia maonesho haya kama fursa ya kujifunza namna bora ya kufuga samaki ikiwemo halmashauri ya Wilaya ya Busega kwani ipo kandokando ya ziwa Viktoria, hii itasaidia pia kupata masoko ya samaki nchini, aliongeza Mhe. Majaliwa.
Kwa upande mwingine Mhe. Majaliwa amezitaka taasisi za kifedha kupunguza riba katika mikopo ili kupata wakopaji wengi Zaidi kutoka sekta ya kilimo nchini. Taasisi hizo ambazo zina mchango mkubwa katika sekta ya kilimo nchini zimetakiwa kuangalia suala hilo ambalo ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo kwani wakulima wengi wanashindwa kuchukua mikopo sababu ya riba ya mikopo hiyo kuwa juu.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa