Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM) ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho Ndg. Daniel Chongolo imefanya ziara ya siku mbili wilayani Busega tarehe 31/01/2022 hadi 01/02/2022 kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo, na kuangalia shughuli za miradi mbalimbali zinazoendelea Wilayani Busega na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi hiyo.
Katika siku ya kwanza ya ziara hiyo Wilayani Busega Naibu Makatibu wa CCM Taifa kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar Ndg. Christine Mndeme na Ndg. Dkt. Abdalah Mabodi wakimwakilisha Katibu Mkuu walitembelea kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Mkula na mradi wa vyumba vya madarasa 14 katika shule ya Sekondari Kabita, madarasa yaliyojengwa chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Mkula ambao ujenzi wake unagharimu kiasi cha TZS milioni 400 na ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la upasuaji na jengo la wodi ya wazazi na ujenzi wa majengo hayo unaendelea. Ukamilikaji wa ujenzi wa kituo hicho utahudhumia zaidi ya wananchi 16,800 wa Kata hiyo na wananchi wa maeneo ya karibu. Ujumbe wa Sekretarieti hiyo umeelekeza kwamba huduma zianze tu pale majengo muhimu yatakapokamilika. “Tungependa kuona majengo haya yaanze kutumika tarehe 28/02/2022 kwa majengo yaliyokamilika mkiendelea kumalizia majengo yaliyobaki ili wananchi wa Mkula waweze kupata huduma” aliongeza Mndeme.
Aidha, Naibu Katibu CCM Taifa upande wa Bara Ndg. Christine Mndeme amewaasa wananchi wa Kata hiyo na Busega kwa ujumla kutumia huduma za hospitali ili kuokoa maisha yao hasa wakina mama. “Tunapaswa kushawishi na kutoa elimu kwa wanachi hasa wajawazito kuja kuhudhuria kliniki na kujifungulia katika vituo vya Afya ili kuokoa maisha ya mama na mtoto” alisema Mndeme.
Halikadhalika, ziara hiyo ilitembelea mradi vyumba vya madarasa yaliyojengwa chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika shule ya Sekondari Kabita ambapo jumla ya TZS milioni 280 imetumika kujenga vyumba 14 vya madarasa. Sekretarieti hiyo imeridhika na ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa ambavyo vimeanza kutumika. Aidha, Mndeme amesema changamoto za vyumba vya madarasa kwa shule za msingi ni jambo ambalo wao kama chama wanaendelea na mikakati ili Serikali iweze kutatua tatizo hilo kama ilivyo kwa shule za sekondari. Kwa upande mwingine ujumbe wa Sekretarieti hiyo imeagiza Halmashauri ya Wilaya ya Busega kuona namna ya kujenga miundombinu katika shule ya msingi Masangani ambayo kwasasa ni shule shikizi.
Katika siku ya pili ya ziara hiyo ujumbe wa Sekretarieti CCM Taifa ilifanya ziara ya kukagua ujenzi wa wodi tatu katika hospitali ya Wilaya ya Busega, ambapo Serikali imetoa kiasi cha TZS milioni 500 kwaajili ya ujenzi wa wodi ya wanaume, wanawake na watoto. Ujumbe wa Sekretarieti ya CCM Taifa iliridhika na mwenendo wa ujenzi wa wodi hizo na kusisitiza kwamba huduma za Afya ziendelee kutolewa kwa ufanisi mkubwa kwani lengo la Serikali ni kufikisha huduma bora kwa wananchi ikiwemo huduma za Afya.
Ujumbe wa Sekretarieti hiyo umeagiza kuharakisha utengenezwaji na uwekaji wa miundombinu ya maji, barabara na umeme katika hospitali ya Wilaya na vituo vya Afya ili kuwezesha huduma bora za Afya. Pamoja na mengineyo, ujumbe wa Sekretarieti hiyo ulipata muda wa kukutana na kuzungumza na baraza la wazee wa Busega ili kusikiliza kero na changamoto zao zinazowakali na kutembelea mashina ya chama hicho.
Uongozi wa Wilaya ya Busega ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria imetoa shukrani kubwa kwa Sekretarieti ya CCM Taifa. “Tutafanyia kazi yote yaliyoelekezwa ili kuondoa changamoto zilizopo” aliongeza Zakaria.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa