Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila amesema ni jambo la msingi viongozi kukutana na Wananchi ili kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili. Ameyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara na Wananchi wa kijiji cha Mwamkara, kilichopo kata ya Nyaruhande Wilayani Busega siku ya tarehe 13/07/2021.
“Ni wajibu wangu kuhakikisha ninawafikia wananchi na kuzungumza nao, kwakuwa Serikali yetu ni sikivu”, amesema Mhe. Kafulila. Amewataka wananchi wa kijiji cha Mwamkara kuwaamini viongozi waliopo katika ngazi zote na wasisite kuwasilisha kero zao kwa Viongozi hao.
Mhe. Kafulila amesikiliza kero za wananchi katika kijiji hicho, ambapo wananchi wameweza kuwasilisha kero zao, zikiwemo uhaba wa maji safi na salama, ukosefu wa miundombinu ya barabara, mgogoro wa ardhi, huduma za afya na uhaba wa watumishi wa kada ya elimu. Mhe. Kafulila amesema amezipokea kero zote na yupo tayari kuwasiliana na mamlaka zinazohusika ili zifanyiwe kazi na zile zinazotakiwa kutatuliwa kwa muda mfupi zitafanyiwa kazi.
Akijibu kero ya ukosefu wa Zahanati katika kijiji hicho Mkurugenzi Mtandaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Bw. Anderson Kabuko, amesema tayari upo mpango wa kujenga kituo cha Afya huku kiasi cha Tshs Milioni 200 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 zimetengwa kwaajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho. Aidha, Kabuko amesema Wilaya ipo katika mpango wa ujenzi wa Shule 24 za Sekondari ifikapo 2025, hivyo kupitia mpango huo utasaidia kupunguza kero ya msongamano wa Wanafunzi katika shule za Sekondari.
Kwa upande mwingine Mhe. Kafulila amesisitiza kutolewaji wa taarifa za fedha zinazojumuisha mapato na matumizi kwa wananchi ili waweze kufahamu matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa. “Taarifa za fedha ziwekwe kwenya mbao za matangazo ili wananchi wajue matumizi ya fedha hizo ikiwemo zile zinazoletwa na Serikali na zile zinazotokana na michnago ya wananchi”, aliongeza Kafulila.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema wananchi wa kijiji cha Mwamkara wanastahili kujipongeza kwa kutembelewa na uongozi wa Mkoa na ameahidi kushirikiana na kijiji hicho ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuwatumikia wananchi. Mhe. Zakaria amesema kikao hicho ni muhimu kwani licha ya kuwa na majukumu waliyonayo viongozi lakini wameweza kufika katika kijiji hicho na kukutana na wananchi ili wasikilize changamoto na kero zao.
Mwisho
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa