Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa kupata hati safi iliyotokana na ufanisi katika utendaji wa majukumu mbalimbali ikiwemo usimamizi wa matumizi wa fedha za Serikali. Kafulila amesema hayo wakati wa Baraza Maalum la Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021, lililofanyika leo tarehe 28 Juni 2022.
“Nawapongeza kwa kupata hati safi nitoe wito kwa uongozi na watumishi wa Wilaya ya Busega kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na maarifa ili kutekeleza lengo la Serikali”, amesema Kafulila. Aidha, Kafulila amewataka watumishi wa Halmashauri kuendelea kuwa na morali na kupenda kazi zao ili kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa halamshauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Ng’habi Mojo amesema licha ya kuwa na mwendelezo wa kupata hati safi lakini amesisitiza kutobweteka kwa watendaji, kwani hali hiyo inaweza kusababisha matokeo mabaya na yasiyoridhisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore amesema tayari hoja zipatazo 24 zimefanyiwa kazi huku hoja 34 zikiendelea kufanyiwa kazi. Awali, Mkaguzi Mkuu wa nje wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Simiyu Gwamaka Mwakyosi amesema katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Wilaya ya ya Busega ilipata maagizo 8 kutoka kwa Kamati ya Bunge ya Ukaguzi wa Serikali za Mitaa (LAAC) na tayari maagizo 3 yamefanyiwa kazi huku mengineyo 5 yakiendelea na utekelezaji wake.
Pamoja na hayo, Kafulila alieleza jinsi alivyoridhishwa na uchapaji kazi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore, huku akiwataka viongozi na watumishi wa Wilaya ya Busega kuendelea kushirikiana nae ili aendelee kutekeleza majukumu yake. “Kiukweli nipende kumpongeza Mkurugenzi kwa kuchapa kazi ya hali ya juu hasa kwa upande wa ukusanyaji na matumizi ya fedha kwani mpaka sasa tayari makusanyo ya ndani yamefikia asilimia 97”, aliongeza Kafulila.
Halikadhalika, Kafulila amesema hana budi kumpongeza Mkurugenzi kwa upande wa fedha za miradi ya maendeleo, fedha zinazotokana na mapato ya ndani ambapo mpaka sasa asilimia 99 imepelekwa kutekelezwa miradi mbalimbali, huku akionesha kufurahishwa na utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa makundi ya wanawake, walemavu na vijana kwani Wilaya ya Busega mpaka sasa imetekeleza kwa asilimia 100.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa