Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ameipongeza Wilaya ya Busega kwa kukamilisha ujenzi wa vyumba 95 vya madarasa ambayo vimejengwa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO 19. Kafulila amesema hayo wakati alipofanya ziara Wilayani Busega siku ya leo tarehe 30 Disemba 2021 kwaajili ya kukabidhiwa madarasa hayo.
Kafulila amesema kuwa ujenzi wa madarasa hayo yote umekamilika na mkoa uko tayari kwa ajili ya kupokea wanafunzi wote ambao watatakiwa kuanza shule huku akizipongeza kamati zote zilizozohusika kusimamia ujenzi huo.
“Nizipongeze kamati zote ambazo zimehusika katika ujenzi wa madarasa haya, mmefanya kazi kubwa sana, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa fedha hizi ambazo zimewezesha ujenzi wa madarasa yote haya,” amesema Kafulila.
Aidha, Kafulila amewataka wananchi kwenye maeneo ambako madarasa hayo yamejengwa kuhakikisha wanayatunza na kuyatumia kwa kazi iliyokusudiwa huku amewataka wananchi kuthamini jitihada kubwa zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo.
“Kimsingi kama Rais asingelifanya hivi, wananchi sasa hivi mgelikuwa mnahangaika kujenga madarasa lakini kwa fedha hizi hamjatoa mchango wowote, na muda huu mnautumia kwa ajili ya maendeleo yenu, lazima tumpongeze Rias wetu na kumshukuru,” aliongeza Kafulila.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema Wilaya ya Busega ilipokea kiasi cha TZS Bilioni 1.9 kutoka Serikali kuu kwaajili ya ujenzi wa vyumba 95 vya madarasa katika shule za Sekondari na shule Shikizi. Ujenzi wa madarasa hayo utasaidia idadi ya wanafunzi 6,297 kujiunga kidato cha kwanza na wanafunzi wapatao 220 kunufaika na madarasa 5 yanayojengwa katika shule moja shikizi ifikapo Januari 2022.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa