Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda amezitaka taasisi za Umma zilizopo mkoani Simiyu kushirikiana kwani zote zinafanya kazi chini ya Serikali moja. Dkt. Nawanda ameyasema hayo alipofanya ziara ya siku moja kutembelea pori la akiba Kijeleshi lililopo wilayani Busega.
Dkt. Nawanda amesema, lengo la Serikali ni kuona huduma zinatolewa kwa wananchi, hivyo taasisi za Umma hazina sababu ya kutoshirikiana katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili. “Tukiwa kama taasisi za Umma ni lazima tuhakikishe tunashirikiana kutatua chnagamoto mbalimbali, tukifanya hivyo tunasaidia wananchi”, aliongeza Dkt. Nawanda.
Awali, Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya Ziwa, SACC. Gisela Kimario amesema kwamba pori la akiba Kijeleshi ni pori ambalo linasaidia sana mzunguko wa wanyama mbalimbali ambao wengi wao wanatoka katika hifadhi ya Serengeti. Kimario anasema uwepo wa pori hilo ni chachu ya utalii kwa wazawa na wageni kwani ni pori lenye wanayama pendwa zaidi na watalii wakiemo Tembo, Simba na Mbuni.
Aidha, Dkt. Nawanda hakusita kuzungumzia suala la wanyama wakali ambao wamekuwa kero kwa wananchi wengi wanaoishi pembezoni mwa pori hilo. Kwa upande wake Kamanda wa pori la akiba Kijeleshi, Lusato Masinde anasema kwasasa wanaendelea na udhibiti wa wanyama hao, wakiwemo Tembo ambao wamekuwa kero katika baadhi ya maeneo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema kupitia utalii Wilaya ya Busega itakua kiuchumi, na kueleza kwamba milango ipo wazi kwa wawekezaji kuja kuwekeza wilayani Busega kwani licha ya pori la akiba Kijeleshi kuwepo Busega lakini Wilaya ipo karibu na lango la Ndabaka, ambalo ndilo langu kuu la kuingia hifadhi ya wanyama Serengeti.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Veronica Sayore amesema Ofisi yake ipo tayari kushirikiana na taasisi zote za Umma ikiwemo TAWA. Sayore amesema atashirikiana na TAWA kuhakikisha changamoto ya wanyama wanaoingia katika makazi ya watu nakuharibu miundombinu wanadhibitiwa.
Katika ziara hiyo Dkt. Nawanda alitembelea ujenzi wa lango la kuingia hifadhi ya Kijeleshi, kituo cha Askari wa kudhibiti wanyamapori wakali, Mwabayanda, na kambi ya Ngulyati. Pori la akiba Kijeleshi lina ukubwa wa kilometa za Mraba 65.7 ambapo lilianzishwa mwaka 1992 huku asilimia 80 ya pori hilo likiwa katika Wilaya ya Busega.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa