Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ametaka uvuvi kuwa fursa ya kimkakati katika kuchochea maendeleo Wilayani Busega. Ameyasema hayo wakati wa Baraza la Madiwani la Kujadili Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka ulioishia 30 Juni 2020 Wilayani Busega, lililofanyika tarehe 24 Juni 2021.
Mhe. Kafulila amesema ni wakati sasa umefika kwa Wilaya ya Busega kuhakikisha inafanya mapinduzi makubwa ili kutumia sehemu ya ziwa Viktoria kuongeza tija ya shughuli za uvuvi. “Mnatakiwa kuhakikisha mnatumia fursa ya uvuvi kuleta kasi ya maendeleo, shughuli ya uvuvi iwe miongoni mwa mikakati muhimu ya Wilaya ya Busega”, aliongeza Kafulila.
Kwa upande mwingine Mhe. Kafulila amesema kipaumbele cha uvuvi na vipaumbele vingine haviwezi kufanikiwa kama hakutakuwa na usimmamizi na muamko wa wananchi. Amewataka wawakilishi wa wananchi, ambao ni madiwani kusimamia vyema Mipango ya Halmashauri kupitia vikao vya mabaraza.”Kuongeza ufugaji wa Samaki kupitia vizimba itaongeza shughuli za uvuvi Wilayani Busega”, alisema Kafulila.
Mhe. Kafulila pia ametaka kuimarika kwa usimamizi wa kilimo cha zao la Pamba, kwani Mkoa wa Simiyu unachangia zaidi ya asilimia 55 ya Pamba yote nchini. Amesisistiza kwamba malengo ya Mkoa kwenye uzalishaji wa zao la Pamba kwa msimu ujao ni kufikia tani 500,000, ambapo itasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri za Mkoa wa Simiyu.
Mhe. Kafulila amesema kwamba ili kufikia malengo ya uzalishaji wa pamba kufikia tani 500,000, ni muhimu kuweka mikakati, ikiwemo kuhakikisha kila mkulima wa zao la Pamba anapatiwa mbolea, hasa mbolea ya Samadi. Kwa upande mwingine Kafulila ametaka kusimamiwa vyema uuzaji wa pamba ili kulinda maslahi ya Wakulima, na kusisitiza kutowaonea haya wote watakaobainika kuhusika na wizi wa ununzi wa Pamba.
Awali, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Simiyu Bw. Gwamaka Mwakyosi, amesema Busega imeendelea kupata hati safi, lakini ametaka uzingatiaji wa matumizi bora ya fedha za Serikali ili kuongeza ufanisi wa shughuli mbalimbali.
Akifungua kikao cha Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe, kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ambae ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu mhe. David Kafulila, aliweza kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ili ajitambulishe, kwani ni mara yake ya kwanza kuhudhuria Baraza hilo tangu ateuliwe katika nafasi hiyo.
Mhe. Gabriel Zakaria amesema anajisikia furaha kuhudhuria kikao cha Baraza la Madiwani na kusisitiza kwamba amekuja kuwatumikia Wananchi wa Wilaya ya Busega kwani yupo tayari kushirikiana na viongozi wa Wilaya ya Busega. Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko amesema Ofisi yake itayafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa ili kufikia malengo ya Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa