Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli atafanya ziara ya siku tatu (03) Mkoani Simiyu, kuanzia kesho tarehe 08/09/2018 hadi tarehe 10/09/2018, Mkoani Simiyu.
Akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Mkuu wa Mkoa Mhe. Anthony Mtaka amesema Mhe. Rais akiwa mkoani Simiyu atapata nafasi ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo, kuweka mawe ya msingi, kufungua pamoja na kuzungumza na Wananchi kupitia mikutano ya hadhara.
Mtaka amesema siku ya Jumamosi tarehe 08/09/2018, Mhe. Rais atakagua na kuweka jiwe la msingi Ujenzi wa Mradi wa Maji wa Lamadi uliopo wilayani Busega na baadaye, ataelekea wilayani Bariadi.
Aidha, amesema Mhe. Rais akiwa katika Wilaya ya Bariadi, atafungua Jengo la Wagonjwa wa Nje(OPD) Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, atakagua na kufungua barabara za lami (kilomita 6.9) zilizojengwa chini ya mradi wa kuboresha Miundombinu ya Miji (ULGSP).
“Siku hiyo pia atakagua maendeleo ya Ujenzi wa barabara ya Bariadi-Maswa inayojengwa kwa kiwango cha lami na kuweka jiwe la msingi. Mhe.Rais atapokea salamu za Chama Cha Mapinduzi, salamu za Wilaya, Mkoa, taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara na baadaye kuzungumza na Wananchi wa Mkoa wa Simiyu na Watanzania wote kwa ujumla, katika Mtaa wa Salunda kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Salunda.”
“Tarehe 09/09/2018 Mhe. Rais atazungumza na wananchi wa wilaya ya Itilima eneo la Makao Makuu ya Wilaya (Lagangabilili) na kuelekea wilayani Meatu. Akiwa njiani kuelekea Meatu Mhe. Rais atapata fursa ya kusalimia wananchi wa Kijiji cha Mwandoya na baadaye atafungua Miundombinu ya Uboreshaji wa Huduma za Afya Hospitali ya Wilaya ya Meatu na kuzungumza na wananchi katika Viwanja vya Stendi ya Mwanhuzi” Alisema Mtaka.
Ameongeza kuwa Siku ya Jumatatu tarehe 10/09/2018 Mhe. Rais Magufuli atahitimisha ziara yake Mkoani Simiyu kwa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja la Mto Sibiti na kuwasalimia wananchi. Daraja la Mto Sibiti ndilo linalounganisha Mkoa wa Simiyu na Singida.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa wito kwa wananchi wote mkoani Simiyu hususani katika Miji ya Lamadi, Bariadi, Lagangabilili, Mwanhuzi na vitongoji vyake kujitokeza kwa wingi katika maeneo yote ambayo Mhe. Rais Magufuli atapita na kufanya mikutano ya hadhara.
Kwa hisani ya http://simiyu.go.tz
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa