Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema wakati umefika kufanya mapinduzi ya kilimo kuwa na tija kubwa, huku akisisitiza kwamba mapinduzi ya kilimo yanahitaji ushirikishwaji na uwajibikaji wa maafisa ugani. Prof. Mkenda amesema wakati akikabidhi pikipiki 86 kwa maafisa ugani kutoka Halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu.
Aidha, Prof. Mkenda amesema licha ya changamoto zilizopo kwenye kilimo, lakini mikakati bora na usimamizi utaleta mapinduzi ya kilimo nchini kwani Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine, Prof. Mkenda amezitaka Halmashauri kuhakikisha zinaweka kipaumbele cha kilimo kwenye bajeti ya kila mwaka. “Halmashauri zihakikishe zinatenga asilimia 20 kwaajili ya shughuli za kilimo, kwa lengo la kuinua kilimo na kuwa na kilimo chenye tija”, aliongeza Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila amesema uongozi wa mkoa wa Simiyu hautakuwa tayari kuona pikipiki hizo kutumika katika shughuli nyingine zaidi ya kilimo. Kafulila amesema yoyote atakaebainika kutumia pikipiki hizo kinyume na lengo atawajibika kwa taratibu za kiutumishi.
Mkoa wa Simiyu una maafisa ugani wapatao 134 huku nchi ikiwa na idadi ya maafisa ugani wapatao 6,704 sawa na asilimia 32.6, huku mahitaji ikiwa ni maafisa ugani 20,538. Tukio la ugawaji wa pikipiki hizo 86 ambazo zimetolewa na bodi ya pamba ikiwa ni juhudi za kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa Mkoa wa Simiyu.
Tukio la ugawaji wa pikipiki limefanyika Wilayani Bariadi limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore, pamoja na wadau wengine wa zao la pamba.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa