Kutoka Busega
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amewapongeza Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa kazi kubwa ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa Wilayani Busega. Zakaria ametoa pongezi hiyo wakati wa kikao cha robo ya pili cha baraza la Madiwani kilichofanyika tarehe 03/03/2022.
“Niwapongeze kwa umakini wenu, maana mmeonesha ni jinsi gani mnafuatilia kwa karibu shughuli mbalimbali zinazoendelea katika Halmashauri na Wilaya kwa ujumla”, alisema Zakaria. Katika kikao hicho ambacho Madiwani waliweza kuhoji mambo mbalimbali ikiwemo fedha za miradi kwa lengo kupata uelewa na ufafanuzi.
Halikadhalika, Zakaria amewakumbusha Madiwani kuhimiza wazazi kuwapeleka shule watoto ambao wamefikia umri wa kuanza shule. “Tuhamasishe uandikishaji wa watoto mashuleni, kwa watoto wote wanaostahili kuwepo shuleni, hii itasaidia kuongeza idadi kubwa ya watoto katika shule zetu na hii ndio dhima kuu ya Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu”, aliongeza Zakaria.
Pamoja na kutambua kazi kubwa inayofanywa na Madiwani, pia Zakaria amewataka Madiwani kuendelea kufuatilia miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili miradi hiyo iwe na ufanisi mkubwa. Aidha, Zakaria amewakumbusha Madiwani kuendelea kuwaeleza wananchi shughuli za miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali katika maeneo yao kupitia mikutano ya hadhara, kwani baadhi ya maeneo kumekuwa na uelewa potofu kuhusu miradi inayoendelea kutekelezwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Mhe. Sundi Muniwe amesema madiwani wataendelea kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kuijenga Wilaya ya Busega. Aidha, kikao cha baraza hilo limeagiza masuala mbalimbali kufanyiwa kazi ikiwemo uharakishwaji wa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati.
Pamoja na hayo, baraza hilo limetaka Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha madeni ya vibarua wa Halmashuari yanalipwa ifikapo mwisho wa mwezi huu ili kumaliza suala la madeni yanayodaiwa na vibarua hao, ambao wengi wao ni wakusanya ushuru wa Halmashauri.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Gidion Bunto anasema mchakato wa malipo ya vibarua unaendelea na muda wowote watalipwa fedha zao kwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa na mchango wao unatambulika. “Tayari tunaendelea na mchakato wa malipo ya vibarua, hivyo watalipwa pale mchakato huo utakapokuwa umekamilika”, alisema Bunto.
Kikao hiki cha robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kimefanyika ikiwa ni utaratibu wa kila robo katika mwaka wa fedha kwa madiwani kukutana na kujadili shughuli mbalimbali zilizofanyika katika robo husika.
Mwisho
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa