Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia masuala ya Afya Dr. Festo Dugange ametoa pongezi kwa uongozi wa Wilaya ya Busega kwa kusimamia vyema miradi ya maendeleo iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa. Dr. Dugange ameyasema hayo alipofanya ziara ya siku moja mapema wiki hii.
Katika ziara hiyo Dr. Dugange alitembelea mradi wa ujenzi wa madarasa katika shule ya Sekondari Mkula, mradi unaotekelezwa chini ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19. Dr. Dugange ametoa pongezi na kusisitiza kwamba kasi ya ujenzi wa miradi ya maendeleo inatakiwa kutekelezwa kwa ufanisi, ubora na kwa wakati.
Dr. Dugange amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba ifikapo Januari mwaka 2022, wanafunzi wote wa kidato cha kwanza wanapata fursa ya kuingia darasani. Aidha, Dr. Dugange amesema hakutakuwa na machaguo tofauti ya wanafunzi watakaojiunga kidato cha kwanza kama ilivyozoeleka hapo awali, bali wanafunzi wote wataingia kwa pamoja kuanza masomo.
Serikali imeipatia Wilaya ya Busega kiasi cha TZS. Bilioni 1.9 kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 95 katika Shule za Sekondari na Shule Shikizi. Mrdai wa ujenzi wa madarasa hayo umefikia zaidi ya asilimia 90 kukamilika kabla ya tarehe 31 Disemba 2021.
Kwa upande mwingine, Dr. Dugange ametembelea ujenzi wa kituo cha Afya Mkula ambao unagharimu TZS Milioni 400 na kuagiza kwamba nguvu zaidi itumike ili kukumilisha mradi huo, kwa lengo la kusogeza huduma zaidi kwa wananchi. Ujenzi wa mradi wa kituo cha Afya Mkula utasaidia kuhudumia zaidi ya wananchi wapatao 16,000. Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Veronica Sayore wameshukuru ujio wa Naibu Waziri na kumhakikishia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa.
Mwisho
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa