Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 zinazoongozwa na mkimbiza Mwenge Kitaiafa mwaka 2022 Ndg. Sahili Nyanzabara Geraruma zimepokelewa Wilayani Busega tarehe 06 Julai 2022 ikiwa ni mapokezi ya Mkoa wa Simiyu na kupitia miradi 9 yenye thamani ya zaidi ya Tshs bilioni 1.83 Wilayani Busega. Halmashauri ya Wiliya ya Busega imekuwa halmashauri ya kwanza kukimbiza mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 kati ya halmashauri 6 zilizopo Mkoa wa Simiyu,
Pamoja na kukagua miradi, Ndg. Geraruma ameweza kutoa maagizo ya kuhakikisha miradi ya maendeleo inasimamiwa vyema sambamba na upatikanaji wa nyaraka za miradi yote inayotekelezwa na Serikali na watu binafsi. Aidha, Geraruma amewakumbusha wananchi wa Busega kujiandaa na kushiriki Sensa ya Watu na Makazi ambayo inatarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti 2022. “Tujiandae kushiriki katika Sensa ili kuhakikisha Serikali inapata tathmini ya idadi ya watu kwaajili ya kupanga mipango endelevu”, aliongeza Geraruma.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi wa kituo cha mafuta cha Ndono kilichopo lamadi, mradi ambao una thamani ya Tshs milioni 385, mradi wa kikundi cha vijana cha kufyatua matofali ambacho kinanufaika na mikopo ya halmashauri yenye riba nafuu ambapo kikundi hicho kimepokea kiasi cha Tshs milioni 18.
Aidha, miradi mingine ambayo imepitiwa na Mwenge wa Uhuru ni mradi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule ya sekondari Shigala, madarasa hayo yamejengwa chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19, mradi ukiwa na gharama ya Tshs milioni 60, mradi wa ujenzi wa kituo cha Afya Ngasamo wenye thamani ya Tshs milioni 500, mardi wa maji Kata ya Badugu wenye thamani ya Tshs milioni 369.8, mradi wa barabara ya Badugu-Lwangwe-Shigala wenye thamani ya Tshs milioni 500.4 na mradi wa klabu ya wapinga Rushwa katika shule ya sekondari Ngasamo wenye thamani ya Tshs 241,000.
Kwa upande mwingine Geraruma ameweza kutembelea mabanda mbalimbali yaliyoandaliwa kwaajili ya kutoa elimu ikiwemo banda la Sensa, banda la Lishe, banda ya TAKUKURU na banda la kupima Virusi vya Ukimwi (VVU) na kupongeza uongozi wa Wilaya ya Busega kwa kusimamia elimu ya kampeni mbalimbali za Kitaifa, hasa elimu ya Sensa.
Wilaya ya Busega imekimbiza Mwenge wa Uhuru kwa umbali wa kilometa 181.5 na kuukabidhi Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Baraidi tarehe 07 Julai 2022 ambapo utakimbizwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa