Mwekezaji Azhar Malik kutoka Nchini Malaysia ameonesha nia ya kuwekeza kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.5 katika mradi mkubwa eneo la pori la akiba la Kijereshi na Ziwa Victoria wilayani Busega Mkoani Simiyu. Sehemu ya uwekezaji huo utahusisha ujenzi wa hoteli ya kitalii, usafirishaji, utamaduni na maeneo mengine yatakayoimarisha utalii na kutoa ajira kwa wananchi, wanaishi wilayani Busega na nje ya wilaya hiyo.
Mwekezaji ambaye amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhan Dau amesema ikiwa kila kitu kitaenda kama kilivyopangwa ikiwemo mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa kuanzia mwezi Januari 2020, huku akisisitiza kuwa utatekelezwa bila kuathiri ikolojia na mazingira ya uhifadhi.
“Nashukuru kwa ushirikiano nilioupata kwa viongozi wa ngazi ya Mkoa wa Simiyu, uongozi wa Wilaya ya Busega na pia namshukuru Balozi Dau kwa namna alivyolisimamia jambo hili tangu likiwa wazo mpaka sasa tunapoelekea kwenye utekelezaji naahidi tu kuwa pale pande zote zitakapofanya maamuzi na mikataba ikisainiwa kwa mujibu wa sheria, mwakani mwezi Januari tutaanza utekelezaji,”alisema Malik
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhan Dau amepongeza uongozi wa Chama na Serikali kwa utayari walioonesha, akisisitiza ushirikiano wa viongozi hao na taasisi zote za Serikali zinazohusika, ili mambo yote muhimu yanayohitajika kufanikisha uwekezaji huo yafanyike mapema kuanzia mwezi Januari mwakani ili utekelezaji uanze.
“Kwa kasi na namna tulivyoanza lile lengo tulilojiwekea kwamba ikifika Januari 2020 mambo yote yanayohusiana na taratibu na kusaini mikataba, yanapaswa yawe yamekamilika na wataalam waje site (eneo la mradi) waanze survey (utafiti) watengeneze master plan(mpango kabambe), ili kabla ya mwezi Juni 2020 hili jambo liwe limeanza,” alisema Balozi Dau.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka amesema Uwekezaji huu utaupambanua Mkoa wa Simiyu, Kanda ya Ziwa na kuupambanua utalii kwenye uso wa dunia, ambapo amebainisha kuwa mradi huu utajibu mahitaji mengi kwenye ajira na kukua kwa maendeleo ya ukanda huo. Kwa upande wa Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mh. Tano Mwera amemshukuru Balozi wa Tanzania nchini Malaysia, Mhe. Dkt. Ramadhan Dau kwa kuwezesha kuleta mradi huo katika wilaya ya Busega na kusisitiza kuwa fursa za uwekezaji zaidi upo wilayani humo.
Kwa upande wao Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) wameahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.
Mradi huu wa uwekezaji katika sekta ya utalii wilayani Busega utatekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza inatarajiwa kugharimu takribani dola bilioni 500 na mpaka kukamilika kwake utagharimu dola za Kimarekani bilioni 2.5.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa