Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ametilia mkazo wa kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la Pamba. Mhe. Zakaria Amesema ni wakati sasa umefika kubadilisha mitazamo ya kilimo cha zao la Pamba Wilayani Busega. Ameyasema hayo wakati wa kikao cha majumuisho ya tathmini ya kampeni ya kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la Pamba, kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Simba wa Yuda na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.
Mhe. Zakaria amesema ni wajibu wa viongozi wa Wilaya kusimamia kwa ukaribu shughuli za kilimo cha Pamba ili kufikia malengo ya Wilaya ya kuzalisha tani 50,000 katika msimu ujao wa kilimo. Mhe. Zakaria amewataka Maafisa Ugani kupitia Idara ya kilimo kuhakikisha suala hilo ni moja ya kipaumbele katika majukumu yao, na kusisitiza kwamba atasimamia kwa ukaribu utekelezaji wake. “Nawategemea wataalam wa kilimo, nina imani kwamba Busega tutafikia lengo la kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la Pamba kwasababu mmepata mafunzo na kanuni bora za kilimo cha zao la Pamba”. Aliongeza Mhe. Zakaria.
Kwa upande mwingine, Mhe. Zakaria ameahidi kutoa pongezi kwa wote watakaozalisha kwa kiasi kikubwa zao la Pamba Wilayani Busega. “Vijiji 5 vitakavyofanya vizuri katika uzalishaji wa zao la Pamba tutavipongeza” alisema Mhe. Zakaria.
Awali, Balozi wa zao la Pamba Kitaifa, Bw. Aggrey Mwanri amesema kilimo cha zao la Pamba kinahitaji usimamizi na kanuni za kilimo, ambazo zitamuwezesha Mkulima kuzalisha kwa tija. Bw. Mwanri amesema kanuni muhimu zikiwemo matumizi ya Mbolea, kupanda kwa kufuata nafasi zilizopendekezwa na wataalam na matumizi ya mbegu bora, ni miongoni mwa mambo muhimu katika kuongeza tija ya zao la Pamba. Aidha, Mwanri amesema kilimo cha Pamba kinaweza kubadilisha maisha ya wananchi wa Busega kiuchumi kama kutakuwa na mkakati madhubuti wa uzalishaji wenye tija.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Burilo Deya amesema tayari mikakati imewekwa ikiwa na malengo ya kuongeza tija ya uzalishaji wa zao la Pamba ikiwemo, Maafisa Ugani kupatiwa mafunzo ya kilimo cha uzalishaji wenye tija wa zao la Pamba, mafunzo yaliyofanyika mwezi wa nne mwishoni mwaka huu katika kituo cha utafiti wa kilimo Ukiriguru kilichopo mkoani Mwanza.
Aidha, Bw. Deya ametaja mikakati mingine ikiwemo kuanzisha mashamba darasa, kuwajengea uwezo Serikali za vijiji kuhusu uzalishaji wa zao la Pamba, kuendelea kuwajengea uwezo viongozi juu ya uzalishaji wa zao la Pamba ikiwemo wawakilishi wa wananchi na kuendelea kushirikiana kwa ukaribu na Wataalam na Bodi ya Pamba katika uzalishaji wa zao hilo. Bw. Deya ameongeza kwamba lengo la Wilaya ya Busega ni kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa kilo 200 kwa ekari kufikia kilo 700 kwa ekari kwa msimu ujao wa kilimo.
Washiriki wa Semina hiyo ya uhamashaji wa kuongeza tija ya zao la Pamba, wamesema ni jambo muhimu sana kwa Wakulima wa zao hilo Wilayani Busega kupata elimu ya uzalishaji wa zao la Pamba, ambayo itawasaidia kuongeza tija katika uzalishaji, hivyo watakwenda kuwa mabalozi wa kilimo cha Pamba. Lengo la Wilaya ya Busega ni kuzalisha tani 50,000, huku lengo la mkoa wa Simiyu ni kuzalisha tani 500,000. Wilaya ya Busega inaendelea na kampeni ya kuongeza tija ya uzalishaji wa kilimo cha zao la Pamba katika ngazi ya vijiji, ambapo mpaka sasa vijiji vipatavyo 23 vimepatiwa mafunzo.
MWANZO.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa