Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano S. Mwera ametaka kutunzwa kwa vyanzo vya maji wilayani Busega. Ameyasema hayo wakati wa mkutano mkuu wa wadau wa maji pamoja na jumuiya za huduma ya maji ngazi ya jamii (CBWSOS) kilichofanyika wilayani Busega.
Mhe. Mwera amewataka wadau wa maji kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kutunza miundombinu ya maji, kwani baadhi ya wananchi wamekuwa wakaidi na waharibifu wa miundombinu ya maji kwa makusudi. Hatuwezi kuangalia uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na baadhi ya wananchi wanaoharibu kusudi miundombinu ya maji na wengine wanafikia hata hatua ya kuiba baadhi ya vifaa kwenye miundombinu ya maji, hili haliwezi kuvumilika, aliongeza Mhe. Mwera.
Katika kikao hicho ambacho kilitoa dira ya huduma za maji wilayani Busega huku Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) ikielezea mafanikio ya miradi mbalimbali ya maji kwa kipindi cha miaka minne huku zaidi ya miradi mikubwa saba (7) ikitekelezwa wilayani Busega na kukiwa na Zaidi ya vituo 550 vya kuchotea maji.
Kwa upande mwingine Mhe. Mwera ametaka miradi ya maji iweze kujiendesha kwa kusimamia vizuri makusanyo ya Ankara za matumizi ya maji, na kuomba miradi ya maji isihusishwe na siasa ili iweze kuwa na ufanisi wa utekelezaji uliokusudiwa na kuimarishwa kwa ulinzi maeneo ya vyanzo na miundombinu ya maji. Miradi mingi ya maji ikionekana kupata uharibifu mkubwa kutokana na shughuli nyingi za kibinadamu hasa shughuli za ufugaji na kilimo.
Huduma za maji wilayani Busega zimeweza kuboreshwa huku watu 16,696 wakiwa wanapata huduma ya maji safi na salama sawa na asimilia 42% ya wakazi wote wilayani Busega. Tunatarajia kuwa na ongezeko la watu watakaounganishiwa huduma ya maji na kuongeza takwimu za watumiaji maji kwani kuna miradi mingi inayondelea kwa sasa ikiwemo upanuzi wa mradi wa maji wa Nyashimo, awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa maji Kiloleli, mradi wa maji Mkula na mradi wa maji Kalago, alisema Kaimu Meneja RUWASA Wilaya ya Busega, Mhandisi Safiel Peter Senzota.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa