Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Dkt. Yahaya Nawanda amewataka wajumbe wa baraza la ardhi Wilaya ya Busega kuwa waadilifu ili kusimamia sheria na haki kwa wananchi wa Busega.
Mhe. Dkt. Nawanda ameyasema hayo wakati wa hafla ya kuwaapisha wajumbe hao iliyofanyika leo tarehe 04/11/2022 katika viwanja vya Nyahanga-Nyashimo. Jumla ya wajumbe 4 waliteuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi Mhe. Dkt. Angelina Mabula kuunda baraza la ardhi wilayani Busega. "Mnatakiwa kuzingatia maadili ili baraza hili liwe kimbilio la wananchi wanyonge", aliongeza Dkt. Nawanda. Nawanda amewakumbusha wajumbe walioapihswa kuishi katika maadili ya baraza la ardhi ikiwemo kutopokea na kuomba rushwa na kutunza siri za baraza hilo.
Dkt. Nawanda ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Busega kwa kuhakikisha huduma mbalimbali zimeletwa karibu ikiwemo ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ambayo awali haikuwepo. Aidha amewataka wananchi wa Busega kumuombea Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazozifanya kuhakikisha huduma zinakuwa karibu na wananchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria, hakusita kupeleka salamu za shukrani za wana Busega kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kusogeza huduma mbalimbali za kwa wananchi. "Mimi na viongozi wenzangu wa Wilaya ya Busega tulifuatilia suala hili na kwakweli mafanikio haya ni kwaajili ya wananchi wa Busega", aliongeza Zakaria.
Awali wananchi wa Wilaya ya Busega walikuwa wakifuata huduma za baraza la ardhi katika Wilaya ya Maswa, huku huduma za Mahakama wakizifuata wilayani Bariadi. Nao wananchi wa Busega wameishukuru Serikali kwa hatua kubwa ya kuleta baraza, hivyo wanaamini migogoro ya ardhi itashughulikiwa kwa wakati.
MWISHO.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa