Kituo cha kulea watoto wenye ulemavu wa ngozi kilichopo kata ya Lamadi Wilayani Busega kimetakiwa kufuata taratibu za malezi ya watoto wenye mahitaji maalum. Kituo cha Bikira Maria Mama wa Mungu kina jumla ya watoto wapatao 70. Mkuu wa mkoa ametoa maagizo hayo, licha ya awali kituo hicho kupewa taratibu za uendeshaji wake kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega.
Mhe. Antony Mtaka amefika kituoni hapo na kusikia changamoto na sintofahamu ya uendeshaji wa kituo hicho ambacho hapo awali kilionekana kina malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi waishio karibu na maeneo hayo na kupelekea uongozi wa Wilaya kutembelea kituo hicho na kugundua baadhi ya changamoto ikiwemo kujiendesha bila ya kusajiliwa pia kutokuwa na wataalam wa ustawi wa jamii kwenye kituo hicho.
Kabla ya ziara ya Mkuu wa Mkoa kituoani hapo, kamati ya Ulinzi na usalama ya Wilaya ya Busega ilitoa maelekezo kituoni hapo jinsi ya taratibu za malezi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi (albino) na utambuzi kwa kufanya usajili. Kwenye ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Busega Mh. Tano Mwera alisisitiza ubora wa malezi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi uendane na uhalisia wa maisha yao ya kila siku. Aliyasema hayo alipotembelea kituoni hapo tarehe 31 Januari 2020 na kusisitiza kituo hicho kisingetambulika kama kisingefata taratibu za uendeshaji na sifa za malezi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi.
Kwa upande mwingine ziara ya Mkuu wa Mkoa kwenye kituo hicho ni msisitizo wa uendeshaji wa kituo hicho kwa utaratibu ambao unakidhi haja ya kuwepo kwa malezi bora kwa watoto wenye mahitaji maalum. “Kituo kina muonekano wa mazingira mazuri lakini kimekosa baadhi ya sifa za utendaji na utaratibu wa malezi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi ndio sababu kubwa ya kufanya ziara ya kukitembelea ili kujiridhisha na baadhi ya malalamiko yanayojitokeza kuhusu kituo hicho” alisisitiza Mhe. Antony Mtaka.
Mbali ya ziara ya awali ya Mkuu wa Wilaya ya Busega, pia Mkuu wa Mkoa ameagiza kuwepo kwa ukaribu baina ya Mlezi wa watoto wa kituo hicho na uongozi mzima wa Wilaya ya Busega, kwani uwepo wa kituo hicho ni msaada mkubwa kwa watoto hao. Amemsisitiza Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoani na Wilaya ya Busega washirikiane na mlezi wa watoto wa kituo hicho ili kuhakikisha kituo hicho kinakidhi hadhi ya kulea watoto, ikiwemo kufanya taratibu za usajili, kushirikiana na mlezi wa watoto wa kituo hicho katika kulinda afya na malezi bora ya watoto hao.
Kwa upande mwingine mlezi wa watoto kituoni hapo, Sister Hellena Ntambulwa ameshukuru uongozi wa serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya kwa kutembelea kituo hicho na ameahidi kushirikiana na uongozi wa serikali ya Wilaya kuhakikisha taratibu za usajili na uendeshaji wa kituo hicho zinakamilika. Hata hivyo mlezi huyo amekiri kutokuwa na ufahamu wa kutosha kwa baadhi ya mambo machache juu ya uendeshaji wa malezi ya watoto hivyo ameahidi kufuata taratibu zinazotakiwa na pia kushirikiana na uongozi wa serikali ya Wilaya kwa lengo la kukidhi mahitaji ya malezi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi.
Kituo cha Bikira Maria Mama wa Mungu kilianzishwa mwaka 2011 na kugundulika kufanya kazi kwa kutofata baadhi ya taratibu licha ya kutakiwa kufuata taratibu kwa kupewa maelekezo mara kwa mara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega jinsi ya kuendesha kituo hicho, lakini bado hakukuwa na mafanikio, hivyo kupelekea Mkuu wa Wilaya kufanya ziara mapema mwezi uliopita tarehe 31 Januari na baadae leo tarehe 4 Februari, Mkuu wa Mkoa Mhe. Antony Mtaka, amefanya ziara ya kujiridhisaha na hali ya sintofahamu ya kituo hicho na kuagiza kufuatwa kwa utaratibu wa uendeshaji malezi ya watoto wenye mahitaji maalum kwenye kituo hicho.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa