Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria, viongozi wengine waWilaya, kwa kushirikiana na Watumishi pamoja na Wananchi wa Busega wameupokea Mwenge wa Uhuru, tarehe 28 Juni 2021. Awali, akiupokea Mwenge wa Uhuru, mapokezi yaliyofanyika katika Kijiji cha Lukungu, Kata ya Lamadi, Mkuu wa Mkoawa Simiyu, Mhe. David Kafulila kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Ali Hapi,amesema Mkoa wa Simiyu upo tayari kukimbiza Mwenge wa Uhuru katika Wilaya zotetano. Wilaya ya Busega imeupokea Mwenge wa Uhuru kutoka Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara.
Salamu za Awali za Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021, Luteni Josephine Paul Mwambashi, ameweza kutoa salamu na ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa wakazi wa Busega. Luteni Mwambashi amesisitiza masuala muhimu ikiwemo matumizi ya malipo ya kietroniki katika ukusanyaji wa mapato kwa ngazi ya Halmashauri, kudhibiti madawa ya kulevya, lishe bora ili kujenga jamii imara na kuendelea kupima maambukizi ya virusi vya Ukimwi ili kuikinga jamii yetu. Luteni Mwambashi amesisitiza matumizi ya TEHAMA katika kuchochea maendeleo kama kauli mbiu ya Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021, inavyosema "TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu, Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji".
Yaliyojiri Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021 Wilayani Busega
Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru zimepokelewa siku ya tarehe 28 Juni 2021 na kupita katika miradi sita kwaajili ya kuzindua, kuweka jiwe la msingi na kutembelea. Akiupokea Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema Wilaya yake imejipanga kikamilifu kuupokea na kuukimbiza Mwenge wa Uhuru katika miradi yote iliyopangwa.
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021 Luteni Josephine Paul Mwambashi amewapongeza Wananchi wa Wilaya ya Busega kwa kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo. “Nawapongeza wananchi kwa kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, Serikali inatekeleza fedha nyingi za miradi lakini Wananchi mkishiriki kikamilifu katika miradi hiyo lazima tuwapongeze, alisema Luteni Mwambashi.
Aidha, Luteni Mwambashi amesisitiza utunzaji wa nyaraka za miradi mbalimbali ili kuonesha uhalisia wa utekelezaji wa miradi hiyo. Amesema ni vyema nyaraka na vilelezo muhimu viambatane na taarifa za miradi. Aidha, Luteni Mwambashi ameweza kutembelea banda la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, TEHAMA na kupata maelezo ya baadhi ya mifumo ikiwemo mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Serikali na mingineyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amewashukuru viongozi na Wananchi wa Wilaya ya Busega kwa kuonesha mshikamano katika mapokezi na ushiriki wao katika Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru.
Miradi ipatayo sita imeweza kupitiwa na Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021 Wilayani Busega kwaajili ya kuzinduliwa, kuwekwa jiwe la msingi na kutembelewa. Miradi hiyo imejumuisha mradi wa Ujenzi Zahanati ya kijiji cha Mkula wenye thamani ya TZS Milioni 104.3, mradi wa ujenzi wa Hotel ya Sandmark wenye thamani ya TZS Bilioni 2.2, mradi wa Maji Nyashimo wenye thamani ya TZS Bilioni 2.287, Club ya Wapinga Rushwa ambapo mpaka sasa thamani yake TZS 80,000, mradi wa Maabara Sekondari ya Antony Mtaka wenye thamani ya TZS Milioni 58.51 na kutembelea mradi wa kisima cha maji ambao ulizinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ili kuangalia maendeleo ya mradi, ambao thamani yake ni TZS Milioni 16.6. Mkuu wa Wilaya ya Busega amekabidhi Mwenge wa Uhuru kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi leo tarehe 29 Juni 2021, kwaajili ya kuendelea na mbio hizo katika Wilaya zingine za Mkoa wa Simiyu.
MWISHO
Kuona Picha Zaidi Bofya Kiunganishi cha Bluu: https://web.facebook.com/Halmashauri-ya-Wilaya-ya-Busega-110384587066130
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa