Naibu Waziri Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Mhandisi Andrea Kundo ameyataka Makampuni ya Mawasiliano ya Simu kuhakikisha wanaboresha huduma za mawasiliano wilayani Busega ili kukidhi haja ya mawasiliano. Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara ya siku moja wilayani Busega siku ya tarehe 5 Januari 2021.
Mhandisi Kundo amesema ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma zilizo bora za mawasiliano ni lazima serikali ichukue hatua thabiti kwa pamoja na wadau wa mawasiliano yakiwemo makampuni ya huduma za mawasiliano ya Simu nchini. “kuna baadhi ya maeneo masafa ya huduma za mawasiliano ya simu ni hafifu sana, ukizingatia kuna minara maeneo hayo, hivyo tunaomba makampuni ya huduma za mawasiliano ya simu kuboresha huduma ya mawasiliano” aliongeza Mhandisi Kundo.
Aidha, Mhandisi Kundo ameyataka makampuni hayo ya mawasiliano ya Simu kuhakikisha ndani ya miezi tisa yanaboresha huduma ya mawasiliano kwa kuweka minara ya simu katika maeneo ambayo bado minara haijawekwa wilayani Busega. “Lengo ni kuwa na mawasiliano thabiti na hiyo ni ndoto na matamanio ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli”, alisema Mhandisi Kundo.
Katika taarifa ya hali ya mawasiliano Wilaya ya Busega iliyosomwa na Afisa TEHAMA wa Wilaya ya Busega Bw. Chrispinus Christian, inaonesha kati ya kata 15 zilizopo wilayani Busega ni kata 3 bado hazina minara ya simu, ambazo ni kata za Lutubiga, Malili na Nyaluhande, hivyo hali hiyo inasababisha maeneo hayo kutokuwa na mawasiliano ya uhakika.
Awali mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Tano Mwera ameomba kuimarishwa kwa mawasilino ya huduma za simu katika Wilaya ya Busega, kwani kutokuwepo kwa ufanisi wa mawasiliano kunaleta changamoto kubwa.
Mhandisi Kundo pia aliweza kutembelea kata ya Nyaluhande ambayo ni moja ya kata 3 wilayani Busega ambazo hazina minara ya mawasiliano ya simu na kukiri kwamba kutokuwepo kwa minara ya simu katika kata hiyo kunaleta changamoto ya mawasiliano na kuyataka makampuni ya simu kuhakikisha wanaweka minara eneo hilo na maeneo mengine yenye mahitaji ili kuwa na ufanisi wa mawasiliano.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa