Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Busega wamewataka Watumishi Wilayani Busega kushiriki katika hatua zote ili kufanikisha ujenzi wa vyumba vya madarasa 95 ambavyo ni Utekelezaji wa mgao wa Fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.
Hayo yamesemwa wakati kikao cha dharula cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kilichofanyika ukumbi mdogo wa Halmashauri leo tarehe 25 Oktoba 2021, kikiwa na lengo la kujadili mustakabali wa matumizi na usimamizi wa Fedha za Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, Fedha ambazo zimetolewa na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Halmashauri zote nchini.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe ametaka uwepo wa ushirikiano baina ya watendaji ngazi zote hasa watakaounda kamati. “Tunakwenda kutekeleza ujenzi wa vyumba vya madarasa 95 katika Wilaya yetu, hivyo wote tunaohusika tunapaswa kushirikiana kila mmoja katika nafasi yake”, aliongeza Muniwe.
Kwa upande mwingine, Madiwani wametaka ushirkishwaji wa karibu wa Watendaji wa Kata katika utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo kwani wamekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya ujenzi katika maeneo yao, hivyo ni vyema kuwashirikisha kwa ukaribu.
Nao washirki wa kikao hicho wamesema imekuwa ni tija kubwa kushiriki kikao hicho na wanaamini utekelezaji wa ujenzi wa madarasa katika Wilaya ya Busega utakamilika kwa wakati uliopangwa.
Akitoa ufananuzi wa mgao, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Melkiad Gaka amesema Halmashauri ya Wilaya ya Busega imepatiwa mgao wa Tshs. Bilioni 1.9, kwaajili ya ujenzi wa madarasa 95 katika shule za sekondari na shule shikizi, na kuongeza kwamba ujenzi wa madarasa hayo unatakiwa kukamilika katika kipindi cha miezi mitatu ili mwezi wa kwanza mwaka 2022 Wanafunzi waweze kuanza masomo.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa