Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Busega wametaka kuwepo kwa usimamizi bora wa Fedha za Miardi zinazotokana na Mapato ya Ndani. Madiwani hao wameyasema hayo wakati wa kikao cha Baraza la kufunga Mwaka kwaajili ya kupokea Taarifa ya Utendaji na Uwajibikaji wa Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 lililofanyika leo tarehe 27 Agosti 2021.
Awali Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe amesema ni vyema kuhakikisha fedha zinazoletwa na Serikali na zile zinazotokana na mapato ya ndani zinatumika kwa wakati ili kutekeleza miradi mbalimbali kwa wakati. Aidha, Mhe. Muniwe ameongeza kwamba usimamizi bora wa fedha za miradi unaenda sambamba na uchapaji kazi wa Watumishi.
Wajumbe wa Baraza hilo wamesema kwamba wanatamani kuendelea kuona Miradi ya Maendeleo inakamilika kwa wakati ili kupunguza adha ya Wananchi kupata huduma. Aidha, Madiwani wamsema kwamba iwapo Asilimia 40 ya makusanyo ya ndani itapelekwa kwa wakati katika Miradi ikiwemo ya Ujenzi wa Madarasa na Zahanati itasaidia kuondoa changamoto kwa wananchi katika baadhi ya maeneo yenye changamoto.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore amesema katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022, tayari bajeti imetengwa kumalizia Miradi ya Maendeleo iliyoanza kutekelezwa. Bi. Sayore ameongeza kwamba tayari kuna juhudi za kuongeza makusanyo ya ndani ili kupata fedha za kutosha zitakazopelekwa kutumika kutekeleza Miradi ya Maendeleo.
Pamoja na hayo, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega wameweza kuipokea taarifa hiyo ya Utendaji na Uwajibikaji wa Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021. Miongoni mwa mambo mengine yaliyoibuka katika Baraza hilo ni pamoja na asiimia 10 ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Walemavu, huku Madiwani wakihoji juu ya uchelewaji wa urejeshwaji wa fedha kutoka kwa wanaofadikia na Mikopo hiyo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Busega Bw. Dismas Ijagala amesema kuna ongezeko kubwa la urejeshwaji wa fedha zilizokopeshwa na hatua mbalimbali zinaendelea kuchukuliwa kwa wote ambao hawarejeshi fedha hizo kwa wakati ikiwemo kuwafikisha katika mamlaka husika ikiwemo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Baraza hilo la kufunga mwaka limefanyika ikiwa ni ishara ya kuanza Mwaka mpya wa Fedha 2021/2022.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa