Tamasha la Utalii maarufu kama Lamadi Utalii Festival, limefanyika Wilayani Busega na kufunguliwa na Mh. Naibu Waziri wa Utalii Ndg. Costantine Kanyasu tarehe 29/12/2019. Tukio hilo lilizinduliwa mapema tarehe 23/10/2019 na Mh. Waziri wa Utalii Dr. Hamis Kigwangwala katika Baraza la Biashara na Uchumi lililofanyika Wilayani Busega, ambapo alituma mwakilishi wake Bi. Gloria Mhambo. Tamasha hilo linatarajia kufanyika kwa siku nne (4) kuanzia tarehe 29/12/2019 mpaka 1/1/2019 na baadae litakuwa endelevu kwa kufanyika kila Jumapili ya mwisho ya Mwezi.
Akiongea wakati wa uzinduzi huo Mh. Naibu Waziri amesisitiza lengo la tamasha hilo ni kutangaza vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana Wilaya ya Busega. Pamoja na hilo pia Lamadi Utalii Festival inalenga kutoa elimu juu ya masuala ya Utalii wa Kiutamaduni, kutoa fursa na ajira kwa wajasiliamali wadogo kupata nafasi ya kuuzia bidhaa zao na pia kupata sehemu ya kujifunza zaidi juu ya masuala mbalimbali ya Utalii.
Kwa upande mwingine Lamadi Utalii Festival inatarajia kutoa fursa kwa wawekezaji kutoka mashirika na taasisi mbalimbali zinazofanya shughuli za Kitalii na Uhifadhi kuja kutoa elimu na kutangaza kazi zao kwa washiriki mbalimbali wanaoshiriki tamasha hilo.
Shughuli ambazo zinabeba dhima nzima ya Tamasha hilo ni pamoja na Ngoma za Utamaduni, Vyakula vya Asili, Uchoraji wa aina ya Tinga Tinga, Uchongaji Vinyago na Bidhaa za Kiutamaduni. “Tamasha hili ni chachu ya kutoa fursa kwa wananchi waweze kujiari kwa kujali elimu ya utunzaji wa mbuga zetu” Alisema Mh. Mkuu wa Wilaya, Tano Mwera.
Lamadi ni moja ya Miji midogo inayopatikana Wilayani Busega, Simiyu, amabapo upo karibu na geti la kuingilia Mbuga ya Wanyama Serengeti na Pori la Akiba Kijereshi. Hivyo ni sababu mojawapo inayopelekea tamasha hilo kupewa jina la Lamadi Utalii Festival. Wilaya ya Busega ni miongoni mwa wilaya zinazopatikana kandokando ya fukwe za Ziwa Viktoria, kwa maana nyingine sehemu hiyo ya fukwe ni moja ya maeneo ya Utalii.
“Tunaamini Lamadi Utalii Festival itaongeza idadi ya watalii wa ndani, uzalishaji wa bidhaa na huduma za kitalii utaongezeka, uboreshaji wa kiuchumi kwa wananchi, kuongezeka kwa wawekezaji na elimu zaidi kuhusu Utalii” alisema Mh. Mkuu wa Wilaya Tano Mwera. Pia ili kufanikisha lengo kuu la tamasha hilo ni muhimu na kuhakikisha idadi ya ualikaji wa wadau wa utalii unaongezeka na pia kushirikiana kwa karibu na Bodi ya Utalii ili kutangaza vivutio vya Kitalii vinavyopatikana Wilayani Busega. Aliongeza Mh. Mkuu wa Wilaya.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa