Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira na kamati ya Elimu, Afya na Maji wilayani Busega zimetembelea miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa wilayani Busega. Kamati hizo zilifanya ziara ya kuangalia utekelezaji miradi maendeleo mbalimbali kati ya tarehe 19 na 20 Januari, 2021. Miradi iliyotembelewa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Stendi ya mabasi ya Wilaya ya Busega, ujenzi wa vyumba vya madarasa na ujenzi wa Bwalo katika Shule ya Sekondari Antony Mtaka.
Mradi wa ujenzi wa Stendi ya mabasi inayoendelea kujengwa wilayani Busega unatarajia kugharimu TZS milioni 47 mpaka kukamilika kwake. Hayo yamesemwa na Mhandisi wa ujenzi wa Wilaya ya Busega Bw. Paul Tumbu wakati wa ziara ya kamati ya uchumi, ujenzi na mazingira ilipotembelea mradi wa ujenzi wa stendi hiyo. Ujenzi unaoendelea katika mradi wa stendi hiyo ni ukamilishaji wa choo cha abiria, eneo na kusimama magari na eneo la wafanya biashara ndogondogo.
Stendi ya mabasi ya Wilaya ya busega inajengwa huku ikiwa ni muendelezo wa mikakati ya kuboresha huduma za usafiri wilayani Busega, huku ikiwa ni muda mrefu Wilaya kutokuwa na Stendi, hali ambayo ilikuwa ni changamoto kwa wasafiri. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko ameeleza kwamba stendi hiyo inajengwa huku ikiwa na mgawanyo wa maeneo ambapo pia imejumuisha eneo la wafanyabiashara ndogo ndogo ili na wao waweze kupata fursa ya kufanya shughuli za kibiashara katika stendi hiyo pale tu itakapoanza kutumika rasmi.Picha: Sehemu ya eneo la Stendi ya Wilaya ya Busega, Mkandarasi akiendelea na Ujenzi.
Kwa upande mwingine, kamati ya Elimu, Afya na Maji imeweza kutembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Skeondari Antony Mtaka na kuweza kuijonea miundombinu iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa. Moja ya changamoto zilizopo katika Shule hiyo ni pamoja na upungufu wa madarasa ambapo shule kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 1,578 huku ikiwa na madarasa 20, lakini uhitaji wa madarasa ukiwa ni madarasa 31.
Picha: Kamati ya Elimu, Afya na Maji ikiwa katika Shule ya Sekondari Antony Mtaka kuangalia miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu katika Shule hiyo.
Hata hivyo ujenzi wa miundombinu ikiwemo vyumba vya madarasa unaendelea na jumla ya madarasa 4 yamefikia hatua ya boma ambapo ujenzi unaendelea. “Sababu tuna upungufu wa madarasa, Wanafunzi wataanza kusomea katika Bwalo huku tukiendelea na umaliziaji wa vyumba vingine vya madarasa” alisema Kabuko. Hata hivyo shule hiyo imeweza kupokea zaidi ya TZS Milioni 196 kutoka Serikalini ambapo fedha hizo zimetumika kutekeleza mradi wa bwalo la chakula 1, vyumba 2 vya madarasa ambavyo vimekamilika na vimeanza kutumika, Ujenzi wa Maabara, na ujenzi wa matundu ya vyoo.
Picha: Muonekano wa Bwalo la Chakula linaloendelea na ujenzi katika Shule ya Sekondari Antony Mtaka.
Miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kutekelezwa wilayani Busega ni miongoni mwa mikakati ya serikali kuhakikisha huduma mbalimbali zinaboreshwa na kusogezwa karibu zaidi na wananchi. Baadhi ya wananchi wamekiri kwamba miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa ni msaada mkubwa sana hasa kwa wananchi wenye kipato cha chini, lakini wameomba miradi mbalimbali ya maendeleo itekelezwe kwa wakati.
Picha: Muonekano wa madarasa 2 yaliyokamilika na tayari yameanza kutumika katika Shule ya Sekondari Antony Mtaka, ambayo yamejengwa kwa mradi wa P4R.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa