Kamati ya Ushauri Wilaya ya Busega (DCC) yapitia na kushauri Rasimu ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2021/2022
Posted on: February 10th, 2021
Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Busega (DCC) imepitia na kushauri rasimu ya bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega ya mwaka wa fedha 2021/2022. Kikao cha kamati hiyo kimefanyika tarehe 9 Februari 2021 katika ukumbi wa Silisos.
Akiongoza kikao hicho Mwenyekiti wa kamati hiyo ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe.Tano Mwera, amewaomba wajumbe kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu bajeti hiyo. Pia amewaomba wajumbe kushauri na kutoa mapendekezo ambayo wanaamini yataleta matokeo chanya ya maendeleo wilayani Busega.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Kabuko amesema, tayari upo mkakati wa kuboresha usimamizi wa vyanzo vya mapato mkakati ambao utaongeza makusanyo kutoka vyanzo vya ndani. “Tumeanza na mkakati wa kuboresha baadhi ya Idara zetu, ambapo tumeanza na Idara za Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika, Idara ya Mifugo na uvuvi na Idara ya Ardhi na Maliasili kwa kuongeza vitendea kazi ili kuwezesha upatikanaji zaidi wa makusanyo ya mapato”, Aliongeza Kabuko.
Pamoja na mambo mengine Bajeti hiyo imejikita katika kuleta matokeo chanya na yenye kugusa maisha ya Wananchi mmoja mmoja. Uandaaji wa Bajeti hiyo umejikita katika miongozo na mipango mbalimbali ikiwemo mpango wa malengo endelevu wa maendeleo wa mwaka 2030, dira ya taifa ya 2025, na mpango mkakati wa Halmashauri. Pia imezingatia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa Bunge Mwezi Novemba, 2020. Mapendekezo ya makisio ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 ni TZS Bilioni 35,175,907,278.
Vipaumbele 17 Vifuatavyo Vimeainishwa katika Rasimu hiyo:
Kuchangia miradi ya maendeleo kwa shughuli zinazoanzishwa na wananchi kama njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi zao.
Kulipa posho za vikao na stahiki za Waheshimiwa Madiwani za kila mwezi.
Ujenzi wa miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari.
Kuendeleza shughuli mbalimbali za Ardhi wilayani.
Kugharamia zoezi la usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya vyanzo vya ndani na kukusanya takwimu kwa kila chanzo.
Kugharamia ujenzi wa masoko ya Masanza, Mwamagigisi, na Nyashimo.
Kuendeleza ujenzi wa stendi ya Nyashimo.
Kuboreha huduma za uvuvi.
Kuhamasisha ufugaji bora na kutoa chanjo za mifugo.
Kuongeza vitendea kazi kama vile pikipiki na magari.
Kuboresha huduma za Afya.
Kugharamia uendeshaji wa Ofisi na vikao mbalimbali vya kisheria.
Kujenga vizimba vya kufugia Samaki ili kujiongezea mapato.
Kuendeleza shughuli za ugani kama kilimo cha mazao ya biashara na chakula na mifugo kwa kuhamasisha wananchi kupanda mbegu bora za Pamba na kuanzisha mashamba darasa ya mazao ya Pamba na Alizeti.
Kutoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali, Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.
Kuboresha usafi wa mazingira.
Kugharamia malipo ya vibarua.
Aidha wajumbe wa kikao hicho walipata fursa ya kushauri maeneo mbalimbali ya Rasimu ya Bajeti. Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe kutoka Vyama vya Siasa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Wakuu wa Idara na Vitengo, Watendaji wa Kata, wawakilishi kutoka Sekta binafsi, Wadau wa Maendeleo, Viongozi wa Dini, na wawakilishi kutoka Taasisi zisizo za Serikali.
Kwa upande mwingine, kamati hiyo imepitia na kushauri Mapendekezo ya Bajeti za taasisi zingine za Kiserikali zilizopo wilayani Busega, ambazo ni Bajeti ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).