Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Busega ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria imeitaka Ofisi ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Busega kuwasimamia vyema Wakandarasi wanaojenga barabara Wilayani Busega ili kuharakisha ukamilikaji wa barabara kwa wakati. Maagizo hayo yametolewa siku ya tarehe 29 Julai 2021 wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kukagua miradi ya barabara kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021.
Kamati hiyo imetembelea barabara takribani 11 zilizopo kwenye mpango wa ujenzi na ukarabati kwa mwaka wa fedha 2020/2021. Kwa kiasi kikubwa kamati hiyo imeridhihswa na ukamilikaji wa barabara hizo lakini imeigiaza Ofisi ya TARURA kuhakikisha ujenzi wa barabara hizo unakamilika ndani ya mikataba iliyowekwa. Kwa upande mwingine kamati hiyo imeridhishwa na barabara zilizotengenezwa kwa kiwango cha Moram, kwani barabara zimeonekana kuimarika na kudumu kwa muda mrefu.
Mhe. Gabriel Zakaria amemuagiza Kaimu Meneja TARURA Wilaya ya Busega Mhandisi Pascal Masali kwamba Wakandarasi wote wanaojenga barabara zilizopo Wilaya ya Busega kufika Ofisini kwake kwaajili ya mazungumzo.
Kwa upande wake Kaimu Meneja TARURA Wilaya ya Busega Mhandisi Paschal Masali amesema baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakifanya kazi kwa kasi ndogo na hii inasababishwa na kutokuwa mitambo ya kutosha. Mhandisi Masalia, amesema barabara nyingi zilizopo kwenye matengenezo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 zimekamilika lakini chache miongoni mwa hizo ujenzi wake unaendelea.
Pamoja na mambo mengineyo, Mhe. Gabriel Zakaria amewataka wananchi wa Wilaya ya Busega kutumia vyema miundombinu ya barabara ili ziweze kutumika kwa muda mrefu. Katika ziara hiyo kamati ya Ulinzi na Usalama imeweza kushuhudia uharibifu wa miundombinu ya barabara, kwani wananchi katika baadhi ya maeneo wamekuwa wakitupa taka katika hifadhi za barabara.
TARURA Wilaya ya Busega imeweza kujenga na kukarabati barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 98.89 kwa gharama ya TZS Milioni 621.7 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 na mpaka sasa Wakandarasi wamelipwa TZS Milioni 327. Huku mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA inatarajia kujenga na kukarabati barabara zipatazo 18 kwa thamani ya zaidi ya TZS Bilioni 2.2, kati ya barabara hizo, 6 ni mpya ambazo zitagharimu TZS Bilioni 1 na zitajengwa kwa kiwango cha Moram kutoka vyanzo mbalimbali vya fedha.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa