Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila amesema Serikali imedhamilia kuanzisha chuo cha Kilimo na Mifugo Mkoani Simiyu. Kafulila amesema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Itwimila B Kata ya Kiloleli Wilayani Busega. Katika kikao hicho cha hadhara wakazi wa Kata hiyo miongoni mwa mambo mengine walitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu uwepo wa chuo katika mkoa wa Simiyu.
Kafulila amesema Serikali imedhamilia kujenga chuo hicho ili kuongeza tija kwa vijana kupata maarifa katika masuala ya kilimo na mifugo. “Hiyo ni fursa kwa vijana wetu wa mkoa wa Simiyu, kwani watapata maarifa na ujuzi kupitia chuo hicho kitakachojengwa Malampaka wilayani Maswa” alisema Kafulila.
“Majengo yanayotumika kwa sasa katika ujenzi wa reli kisasa (SGR) maeneo ya Malampaka baada ya kukamilika mradi huo majengo hayo yatatumika kama chuo cha Kilimo na Mifugo”, aliongeza Kafulila.
Aidha, Kafulila amesema kwamba Serikali pia imetenga fedha kwaajili ya kujenga chuo cha ufundi stadi (VETA) mkoani Simiyu na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi wa sita mwaka huu. Kafulila amesema hayo akijibu swali lililoulizwa na mwananchi ambalo lilitaka kujua mpango wa Serikali kuhusu chuo cha ufundi stadi katika mkoa wa Simiyu.
Katika ziara hiyo Kafulila ameweza kusikiliza changamoto na kero za wananchi, miongoni mwa kero hizo ni pamoja na uvamizi wa wanyama katika makazi ya wananchi wakiwemo viboko. Wananchi hao wamesema uvamizi wa viboko katika makazi ya wananchi na maeneo ya mashamba imekuwa ni kero kubwa maeneo tofauti katika Kata hiyo. Kafulila amewatoa hofu wakazi wa Kata hiyo kwa kuwaeleza kwamba suala hilo lipo katika utaratibu wa kuhakikisha kero hiyo inapatiwa mwarubaini wake.
Kwa upande mwingine Kafulila ameweza kutumia fursa ya kikao hicho kueleza masuala machache miongoni mwa mengi yanayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita. Kafulila amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutekeleza miradi yote iliyoanzishwa katika awamu ya tano ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa daraja la Busisi-Kigongo, ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingineyo. Aidha, Kafulila amesema kwa kujali manufaa ya wananchi Serikali ya awamu ya sita imeweza kujenga madarasa 15,000 nchi nzima kwa shule za sekondari na shule shikizi, ambapo kwa mkoa wa Simiyu vyumba vya madarasa 449 vimeweza kujengwa.
Akitoa ufafanuzi wa huduma ya gari la maji taka, Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema taratibu za gari hilo zinaendelea na kikubwa kwasasa ni uandaaji wa miundombinu ili kuweka mazingira bora ya huduma hiyo. Kwa upande mwingine Kafulila ametoa ufafanuzi wa gharama za bei ya uunganishaji wa umeme huku akisisitiza kwamba maelekezo ya Serikali yanataka maneneo yote ambayo ni ya vijijini gharama ya kuunganisha umeme ni TZS 27,000. “Sehemu kubwa ya mkoa wa Simiyu ni vijijini hivyo uunganishwani wa umeme unabaki kama ilivyo awali isipokuwa maeneo ambayo ni ya miji kama ilivyo Bariadi mji na maeneo mengine machache.
Wananchi waliohudhuria kikao hicho wameipongeza Serikali kwa maono ya kuanzisha chuo cha Kilimo na Mifugo kwani vijana wengi wa ndani ya mkoa wa Simiyu na maeneo mengine ya nchini watapata fursa ya maarifa na ujuzi katika sekta ya Kilimo na Mifugo. Halikadhalika wananchi hao wameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, shule na mahospitali.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa