Zaidi ya Bilioni 2.245 zinatarajia kutumika kujenga barabara za vijijini Wilayani Busega. Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Mwita Muhochi katika kikao kilichofanyika siku ya tarehe 24/01/2022 kwaajili ya kupitia utekelezaji wa miradi ya barabara kwa mwaka 2021/2022 na kupitia mapendekezo ya mpango wa mwaka 2022/2023 kwa wadau wa barabara.
Katika kikao hicho, Mhandisi Muhochi amesema kwamba Serikali imeleta kiasi hicho ili kuhakikisha barabara za vijijini zinajengwa kwa ubora ili kuondoa changamoto za miundombinu ya barabara Wilayani Busega.
Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan ina malengo makubwa ya kuhakikisha barabara zinajengwa maeneo mbalimbali kwa ubora unaotakiwa. Aidha, Zakaria amesme licha ya Serikali kuleta fedha hizo ni vyema watekelezaji kuwa na usimamizi mzuri ili ziweze kutumika kwa ufanisi mkubwa. “Niwapongeze TARURA kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya lakini ni muhimu Wakandarasi tunaowapa kazi wawe na uwezo wa kufanya kazi, kwani baadhi wamekuwa na shida ya kutokamilisha miradi ya ujenzi wa barabara kwa wakati” alisema Zakaria.
Kutowapa nafasi Wakandarasi wanaochelewesha kazi ni miongoni mwa mambo yaliyo jadiliwa kwa kina katika kikao hicho, huku wadau mbalimbali wakikiri kwamba kuna baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakichelewesha ujenzi wa miradi ya barabara hivyo kusababisha adha kwa wananchi wa maeneo husika.
Aidha, Zakaria amewataka TARURA kushirikiana na madiwani katika miradi ya ujenzi wa barabara ili kuleta tija ya utekelezaji wa miradi hiyo katika maeneo husika. “Madiwani wakishirikishwa ipasavyo itasaidia kuleta tija na vipaumbele katika maeneo husika”, aliongeza Zakaria.
Wadau walioshiriki kikao hicho wanasema kwamba kazi kubwa imefanywa na TARURA kwani kwasasa sehemu kubwa ya Wilaya inafikika ukilinganisha na hapo awali. Aidha, wameomba barabara ambazo bado hazijasajiliwa kwenye mtandao wa barabara zisajiliwe ili ziweze kufunguliwa, na barabara zote ambazo zina umuhimu mkubwa kwa uchumi wa wananchi kupewa kipaumbele katika matengenezo. Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Mhe. Sundi Muniwe amesema kwamba madiwani wataendelea kushirikiana na TARURA ili kuhakikisha barabara zinajengwa kwa ufanisi mkubwa.
Mtandao wa barabara Wilayani Busega ni kilomita 511 huku kilometa 159.73 sawa na asilimia 31 zipo katika hali nzuri, kilometa 124.01 sawa na asilimia 25 zipo katika hali ya wastani na kilometa 227.36 sawa na asilimia 44 bado zipo katika matengenezo ya awali, wakati asilimia 35 ya barabara zilizotengenezwa zipo katika kiwango cha changarawe (moram) na asilimia 65 ni barabara za udongo. TARURA Wilaya ya Busega inatarajia kutengeneza barabara zipatazo 30 zenye urefu wa zaidi ya kilometa 68.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa