Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ametoa wito kwa watendaji na wasimamizi wa miradi kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa na Serikali. Zakaria amesema hayo wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Halmashauri na ujenzi wa miundombinu katika hospitali ya Wilaya ya Busega leo tarehe 08 Juni 2022.
“Najua tumepokea fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, hivyo tujitahidi kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati”, aliongeza Zakaria. Aidha, Zakaria ametaka fedha zote ambazo zimetengwa kwaajili ya mradi husika zitumike kikamilifu bila kubadilishiwa matumizi.
Utekelezaji wa ujenzi wa jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Busega umefikia zaidi ya asilimia 90, ambapo jengo hilo lenye thamani ya TZS bilioni 4.9 likikamilika litakuwa jumla ya vyumba 97 tayari limeanza kutumika kwa baadhi ya vyumba vilivyokamilika tangu mwishoni mwa mwaka 2020.
Aidha, mradi wa ujenzi wa wodi mbili za upasuaji wa kiume na kike, jengo la kuhifadhi maiti (mortuary), na jengo la upasuaji (theatre), majengo yanayojengwa katika hospitali ya Wilaya, ujenzi wake umeanza na jumla ya TZS milioni 800 ambazo zimeletwa na Serikali zinatarajiwa kukamilisha ujenzi wa majengo hayo.
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa