Mkuu wa wa Wilaya ya Busega Mhe. Gabriel Zakaria ameyataka makampuni yanayonunua Pamba Wilayani Busega kuhakikisha wanalipa madeni ya tozo na kodi za Serikali ifikapo tarehe 10 Oktoba 2021. Zakaria ameyasema hayo wakati wa kikao na wadau wa Pamba Wilayani Busega kilichofanyika tarehe 16/09/2021 katika ukumbi wa Shule ya Msingi Nyashimo.
“Kampuni zote zenye madeni ya kodi zilipe madeni yao ifikapo tarehe 10 Oktoba 2021, kwani miongoni mwa kampuni hizo zimekuwa zikisumbua sana katika ulipaji kodi ambao unakusanywa na Halmashauri”, aliongeza Zakaria.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bi. Veronica Sayore ameyataka makampuni yenye madeni kufika Ofisini kwake kuhakiki madeni hayo kwaajili ya kulipa.
Aidha, Katika kikao hicho suala la kuongeza tija ya Uzalishaji wa zao la pamba lilichukua nafasi, pamoja na mengineyo suala la kuhakikisha mbolea inafika kwa wakati kwa wakulima lilijadiliwa, huku wadau wa pamba wakitaka uwepo wa ushirikiano baina ya mkulima, vyama vya Msingi vya ushirika (AMCOS) na makampuni yanayonunua Pamba.
Afisa kilimo Wilaya ya Busega Bw. Juma Chacha amezitaka kampuni zinazonunua Pamba Wilayani Busega kushirikiana kwa ukaribu na wakulima hasa kwenye suala la upelekaji wa mbolea mashambani kwani wakulima wengi wameshindwa kufikisha mbolea mashambani kutokana na kutokuwa na uwezo wa kufanya hivyo.
Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni Utekelezaji wa mikakati ya kuongeza tija ya zao la Pamba Wilaya ya Busega kwa kuzalisha tani 50,000, huku Mkoa ukiweka lengo la kuzalisha tani 500,000. Mikakati hiyo iliwekwa tarehe 22/08/2021 Wilayani Meatu wakati wa majumuisho ya kampeni ya kuongeza tija ya zao la Pamba iliyofanyika Mkoa wa Simiyu.
MWISHO
Mkurugenzi Mtendaji, Halmashauri ya Wilaya ya Busega
Sanduku la Posta: 157 BUSEGA
Simu ya Mezani: +255 282 981 193
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: info@busegadc.go.tz
Haki Miliki @2019. Halmashauri ya Wilaya ya Busega. Haki zote zimehifadhiwa